May 15, 2022 07:58 UTC
  • Mrithi wa Ufalme wa Saudia akutana na kufanya mazungumzo kwa siri na Mkuu wa CIA

Mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia Mohammad bin Salman amekutana na kufanya mazungumzo kwa siri na Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA William Burns, ambapo wawili hao wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu hali ya soko la mafuta pamoja na uamuzi wa Riyadh wa kutaka kununua silaha kutoka China.

Kituo cha habari cha Arabi21 kimeinukuu tovuti ya habari ya Marekani ya The Intercept na kuripoti kuwa, Burns na Bin Salman wamekutana na kufanya mazungumzo hayo ya faragha mjini Jeddah, Saudi Arabia.

The Intercept imezinukuu duru za kuaminika zikieleza kuwa, mkutano wa mrithi wa ufalme wa Saudia na Mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani umefanyika huku maafisa wa ngazi ya juu wa Washington wakifanya kila njia kuirai Riyadh ikubali kuongeza kiwango cha uzalishaji mafuta na kughairi uamuzi wake wa kutaka kununua silaha kutoka China.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika mazungumzo hayo, Mkuu wa CIA ametilia mkazo pia ulazima wa kuachiwa huru jamaa wote wa aila ya kifalme ya Saudia waliowekwa kizuizini na mamlaka za Riyadh.

Hayo yanajiri katika hali ambayo wiki iliyopita, Saudi Arabia ilisisitiza kuwa itaendelea kuzalisha mafuta kulingana na kiwango ilichojiwekea na kutokubaliana na wito uliotolewa na Marekani wa kuitaka iongeze kiwango cha uzalishaji.

Ripoti ya The Intercept imeongeza kuwa, baada ya mazungumzo ya kujadili uamuzi wa Saudia wa kununua makombora ya balestiki kutoka China, William Burns alimtaka Mohammad Bin Salman asinunue silaha na zana za kijeshi kutoka Beijing.

Kuhusu wanawafalme wa Saudia waliowekwa kizuizini, Mkuu wa CIA amemtaka Mohammad bin Salman ahakikishe Mohammad bin Nayef, mrithi wa zamani wa ufalme pamoja na wanawafalme wengine ambao wamekamatwa na kuwekwa kizuizini na mrithi huyo wa ufalme tangu mwaka 2017 waachiliwe huru.../