May 16, 2022 07:37 UTC
  • Matokeo ya karibuni ya uhesabuji kura za awali katika uchaguzi wa bunge Lebanon

Ripota wa televisheni ya al Aalam ametangaza kuwa, Harakati ya Amal inayoongozwa na Nabih Berri Spika wa Bunge la Lebanon imetangaza baada ya kujulikana matokeo ya awali ya uhesabuji kura kwamba, hadi sasa imeshinda viti 17 bungeni huku Harakati ya Muqawama ya nchi hiyo Hizbullah pia ikishinda viti 23 hadi sasa.

Uchaguzi wa Bunge Jipya la Lebabon ulifanyika jana Jumapili; na hadi sasa zoezi la kuhesabu kura lingali linaendelea na matokeo ya mwisho bado hayajatangazwa. 

Ripota wa televisheni ya al Aalam yenye makao yake hapa Tehran ameeleza kuwa, matokeo ya awali yanabainisha ushindi aliopata mmoja wa wagombea wa mrengo wa kushoto katika eneo la kusini mwa nchi hiyo huku Orodha ya Asasi za Kiraia na Mabadiliko ikishinda katika majimbo mbalimbali.  

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya wafuasi wa Harakati ya Hizbullah na washirika wao wa Kishia yaani Harakati ya Amal wamesherehekea mitaani baada ya kutangazwa matokeo hayo ya awali yasiyo rasmi ya kuibuka washindi baadhi ya wagombea wao. 

Wakati huo huo gazeti la al Nahar lililopo karibu na wapinzani wa muqawama limeripoti kuwa, wafuasi wa Harakati ya  Hizbullah na mshirika wao wa Kishia yaani Harakati ya Amal wameonekana wakiwa wamepanda pikipiki na magari huku wakipiga nara na shaari wakifurahia ushindi huo katika mitaa mbalimbali ya Lebanon.  

Baada ya kumalizika zoezi la kupiga kura katika uchaguzi wa bunge wa Lebanon jana Jumapili, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ametangaza kiwango cha wastani cha ushiriki katika uchaguzi huo kuwa kilikuwa karibu asilimia 41. 

Upigaji kura katika uchaguzi wa Bunge Lebanon 

 

Tags