May 16, 2022 10:51 UTC
  • Ndege ya kwanza ya biashara yapaa kutoka Sana'a baada ya kupita miaka 6

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, ndege ya kwanza ya kibiashara imepaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a kuelekea nchini Jordan baada ya kupita miaka 6.

Televisheni ya al Jazeera imetangaza habari hiyo leo Jumatatu na kuongeza kuwa, baada ya kupita miaka 6 ya kusimamishwa safari za ndege kutoka Sana'a, mji mkuu wa Yemen, hatimaye ndege ya kwanza ya kibiashara imepaa kutoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a kuelekea Jordan.

Muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia uliivamia Yemen mwezi Machi 2015 yaani zaidi ya miaka saba iliyopita na kufunga njia zote za kuingia nchini Yemen, angani, ardhini na baharini kwa tamaa ya kumaliza vita hivyo katika kipindi kifupi tu.

Wavamizi wakiongozwa na Saudia wamefanya jinai kubwa mpaka misikitini huko Yemen

 

Hata hivyo muqawama wa wananchi wa Yemen umewafedhehesha kabisa wavamizi hao ambao wanapewa silaha za kila namna na madola ya kibeberu ya Magharibi baada ya kupita miaka saba bila ya wavamizi hao kufanikisha malengo yao walioyadai kuanzishia vita huko Yemen.

Mwezi Aprili mwaka huu Umoja wa Mataifa ulitoa pendekezo la kusimamisha vita huko Yemen. Pendekezo hilo lililokubaliwa na pande zote, liliruhusu kuingia meli 18 za mafuta katika bandani ya al Hudaidah na kuruhusu safari mbili za ndege za kwenda na kurudi kila wiki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a.

Uvamizi wa kijeshi wa Saudia na kundi lake huko Yemen umeshaua na kujeruhi mamia ya maelfu ya wananchi wa Yemen na kuwafanya wakimbizi zaidi ya Wayemen milioni nne.