May 16, 2022 10:53 UTC
  • Miaka 74 baada ya Siku ya Nakba

Miaka 74 iliyopita, utawala haramu na bandia wa Kizayuni wa Israel ulitangaza uwepo wake baada ya kufanya jinai kadhaa za kinyama dhidi ya Wapalestina.

Kwa Wapalestina, tarehe 15 Mei mwaka 1948 ni "Siku ya Nakba" na kielelezo cha kuhamishwa kwa nguvu na Wazayuni katika makazi yao ya asili wananchi hao wanaoendelea kudhulumiwa hadi leo. Kwa mtazamo wa Wapalestina, Siku ya Nakba ni kumbukumbu ya masiku machungu ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi zao, kuporwa ardhi hizo; na kwa mara ya kwanza kushuhudiwa wimbi kubwa la Wapalestina laki nane waliohamishwa kwenye nyumba na makazi yao na kulazimika kuwa wakimbizi.

Wapalestina walipolazimika kuyahama makazi yao kutokana na unyama wa Wazayuni

Miaka 74 imepita ya jinai hiyo iliyofanywa na utawala haramu wa Kizayuni. Si joto la machungu waliyopata Wapalestina ambalo limepungua, wala si jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Kizayuni ambazo zimekoma na kufikia tamati. Walid al Qat'at'i, mjumbe mwandamizi wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amefanyiwa mahojiano maalumu na shirika la habari la Iran Press akiwa Ukanda wa Gaza na akasema, wananchi wa Palestina wanaendelea kuhimili mateso na machungu ya uvamizi, kugeuzwa wakimbizi pamoja na dhulma na uonevu wanaofanyiwa na Uzayuni wa kikoloni unaoungwa mkono na Magharibi.

Jinai za utawala ghasibu wa Israel zingali zinaendelea. Katika miaka 74 iliyopita, zaidi ya asilimia 85 ya ardhi ya Palestina imevamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni, ikiwa ni sawa na kilomitamraba 27 elfu za ardhi hiyo. Pamoja na hayo, utawala huo ghasibu ungali unaendeleza ujenzi haramu wa vitongoji na ungali una uchu na tamaa ya kupora ardhi na nyumba zaidi za Wapalestina.

Taswira za jinsi Wazayuni walivyopora ardhi za Palestina hadi leo

Katika kipindi cha miaka 74 iliyopita, Wapalestina zaidi ya laki moja wameuliwa shahidi ndani na nje ya ardhi ya Palestina. Pamoja na hayo, wananchi hao madhulumu wangali wamesimama imara kupigania nchi yao ya Palestina na wanaendelea kupambana na utawala dhalimu wa Kizayuni. Vita vya kupambana na utawala huo ghasibu havipambanui wala kutafautisha baina ya mwanamke na mwanamme, mtoto mdogo, kijana au mzee wa Kipalestina. Utambulisho wa Palestina tu unatosha kwa ajili ya kuingia vitani kupambana na Israel. Mfano wa hilo ni Shireen Abu Akleh, mwanahabari Mpalestina wa televisheni ya Aljazeera ambaye aliuliwa shahidi hivi majuzi kwa makusudi na utawala haramu wa Israel wakati alipokuwa anaakisi na kuripoti jinai za kinyama za utawala huo katika kambi ya wakimbizi Wapalestina ya Jenin.

Miaka 16 tangu Ukanda wa Gaza ulipoanza kuwekewa mzingiro imepita. Gaza imegeuzwa jela kubwa zaidi ya eneo la wazi duniani, huku watu wa eneo hilo wakikabiliana na changamoto kali za usalama, afya na chakula. Pamoja na hayo, Wapalestina wa Gaza wangali wamesimama imara kukabiliana na jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni.

Hali mbaya ya kibinadamu Ukanda wa Gaza iliyosababishwa na mzingiro wa Israel

Ijapokuwa mihimili miwili kinzani ingali inashuhudiwa Palestina, ambayo ni ya Muqawama na msimamo wa kufanya mapatano ilionao Mamlaka  ya Ndani ya Palestina bila kujali jinai za utawala haramu wa Israel, lakini kadiri siku zinavyopita ndivyo inavyozidi kubainika kuwa Muqawama ndiyo njia sahihi na ya haki inayopasa kufuatwa kwa ajili ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni; na leo hii utawala huo katili umedhoofika na unatapatapa mbele ya Muqawama wa Wapalestina. Operesheni za mashambulio ya kushtukiza ya Wapalestina ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, ambazo hadi sasa zimeshawaangamiza na kuwajeruhi Wazayuni wasiopungua 19, ni ushahidi wa wazi na wa mbele ya macho unaothibitisha ubora wa muelekeo wa muqawama badala ya mapatano; na ni ithbati kwamba utawala ghasibu wa Kizayuni sasa umeemewa na kuchanganyikiwa. Na ni kwa msingi huo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeeleza katika taarifa iliyotoa kwa mnasaba wa mwaka wa 74 wa Siku ya Nakba ya kwamba, muqawama wa hali na pande zote, hususan wa mtutu wa bunduki, ndio njia pekee ya kujikomboa na ukaliaji ardhi kwa mabavu, kukabiliana na jinai za Wazayuni na kurejesha haki zilizoporwa za taifa la Palestina.

 

Wanamuqawama wa Palestina

Nukta ya kuhitimishia uchambuzi huu ni kwamba, kuasisiwa kwa utawala bandia wa Kizayuni mwaka 1948 kulifanyika kwa msaada na uungaji mkono wa kila hali wa Magharibi; na baada ya kupita miaka 74, Magharibi ingali inaendelea kuuhami utawala huo haramu ulioko kwenye kitovu cha ukanda wa Asia Magharibi na inahesabika kuwa mshirika wa jinai unazofanya. Kimya na uungaji mkono wa Magharibi, ni sababu muhimu ya kuendelea kushuhudiwa jinai za utawala wa Kizayuni. Katika mahojiano aliyofanyiwa na mwandishi wa habari wa Iran Press, Walid al Qat'at'i amesema: "Magharibi ya Kikoloni ilikuwa nyuma ya pazia la uundwaji wa utawala bandia wa Israel (Siku ya Nakba); na jinai ya Nakba ingali inaendelea katika ardhi ya Palestina. Dhima ya kuendelea jinai ya Nakba inabebwa na jamii ya kimataifa, kwa kuruhusu kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Kiislamu na Kiarabu ya Palestina.../

Tags