May 17, 2022 07:26 UTC
  • Amir Abdollahian: Uhusiano mzuri baina ya majirani unawakatisha tamaa maadui katika eneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria mazungumzo kati yake na Rais mpya wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), na kueleza kuwa uhusiano mwema kati ya nchi jirani ni sababu ya kuvunjika moyo maadui katika eneo.

Hossein Amir- Abdollahian ameandika leo katika ukurasa wake wa twitter kwamba: "Ukurasa mpya umefunguliwa katika uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Imarati, tunapeana mkono kwa uchangamfu na majirani zetu. Uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi jirani unawakatisha tamaa maadui."   

Amir Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye alikuwa ameelekea Abu Dhabi kwa minajili ya kutoa mkono wa taazia na rambirambi kufuatia kifo cha Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu jana Jumatatu alikutana na Muhammad bin Zayed Rais mpya wa Imarati ambapo pande mbili hizo zimejadili kuhusu masuala mbalimbali ya pamoja.  

Ajenda kuu ya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Rais mpya wa Imarati ilihusiana na baadhi ya masuala yanayoungwa mkono na pande mbili na yale ya pamoja likiwemo pia suala la kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili raia wa Iran wanaoishi Imarati.  

Baraza Kuu la Imarati Jumamosi iliyopita lilimchagua Mohammed bin Zayed kuwa Rais mpya wa Umoja wa Falme za Kiarabu kufuatia kifo cha Sheikh Khalifa bin Zayed. 

Sheikh Khalifa bin Zayed, aliyekuwa Rais wa Imarati

 

Tags