May 17, 2022 07:44 UTC
  • Saudia: Tuna hamu ya kuzungumza na Iran kuhusu kisima cha gesi cha Arash

Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia amesema kuwa nchi yake na Kuwait zina hamu ya kuzungumza na Iran kuhusu kisima cha gesi cha Arash au al Durra.

Kuwait na Saudi Arabia tarehe 21 Machi mwaka huu zilisaini hati kwa ajili ya kuendeleza kisima cha gesi cha Arash; ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Kampuni ya Mafuta ya Kuwait ilitabiriwa kwamba kisima hicho kwa siku kingezalisha futi za ujazo bilioni 1 za gesi na mapipa 84,000 gesi oevu. Abdulaziz bin Salman Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia amesema katika Mkutano wa 29 wa Mafuta na Gesi wa Mashariki ya Kati uliofanyika Bahrain kuwa: Riyadh na Kuwait ziko tayari kufanya mazungumzo na Iran kuhusu kisima cha gesi cha Arash au jwa jina jingine al Durra. 

Katika mkutano huo, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia amesemam kuwa, Kuwait na nchi yake zinataka kufanya mazungumzo na Iran kuhusu kisima hicho cha gesi kwa sababu maliasili zilizopo huko ni kati ya maslahi ya pamoja ya nchi mbili. 

Baada ya matamshi haya ya Waziri wa Nishati wa Saudia, Saeed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia ametoa radiamali kufuatia mapatano hayo tajwa na kueleza kuwa kisima cha gesi cha Arash au al Durra ni kisima cha pamoja kati ya Iran, Kuwait na Saudi Arabia na kwamba baadhi ya sehemu za kisima hicho ziko katika mipaka ya Iran na Kuwait.   

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kimataifa, hatua yoyote ya kunufaika na kuendeleza kisima hicho inapasa kufanyika kwa uratibu na kushirikiana nchi zote tatu; hata hivyo kitendo cha karibuni cha Kuwait na Saudia cha kutia saini hati ya ushirikiano kati yazo ni kinyume na utaratibu uliopo na mazungumzo yaliyofanywa huko nyuma.

Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran 

Amesema hatua hiyo ya Kuwait na Saudia ni kinyume cha sheria na haijaidhinishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.