May 18, 2022 07:47 UTC
  • Khalid Mash'al: Palestina haitaruhusu kutekelezwa njama za kuiyahudisha Masjdul-Aqswa

Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) nje ya nchi amesisitiza kuwa, Msikiti wa al-Aqswa ni eneo la kidini na ni la Kiislamu kikamilifu na kwamba, wananchi wa Palestina hawataruhusu kutekelezwa njama chafu za kuliyahudisha eneo hilo takatifu.

Khalid Mash'al, Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) nje ya nchi amebainisha kwamba, wananchi wa Palestina wako imara na katu hawataruhusu Masjidul-Aqswa ifanywe kuwa ni ya Mayahudi iwe ni kwa kuligawa eneo hilo au kulibomoa.

Bwana Mash'al ameeleza kwamba, mipango michafu ya Wazayuni ingalipo hivyo amewatahadharisha wananchi wa Palestina kwamba, vita na makabaliano bado hayajaisha kwani katika siku za usoni inatarajiwa Wazayuni watavamia tena Msikiti wa al-Aqswa katika minasaba siku za usoni.

Walowezi wa Kizayuni wakivamia Msikiti nwa al-Aqswa

 

Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) nje ya nchi ameongeza kuwa, adui Mzayuni anajidanganya kwa kudhani kwamba, kuzuia muqawama wa silaha katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kutaandaa uwanja wa kuendelezwa ujenzi wa vitongojii haramu vya walowezi wa Kizayuni na hivyo kutwaa ardhi na kuwa na udhibiti kamili kwa Masjidul-Aqswa.

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala haramu wa Israel umeshadidisha njama zake dhidi ya Wapalestina na hasa katika msikiti wa al-Aqswa sambamba na kuongeza kasi ya ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

Hatua hizo zinakwenda sambamba na kuongeza jinai za utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina huku Umoja wa Mataifa na baraza lake la usalama zikishindwa kuchukukulia hatua utawala huo unaotenda jinai na mauaji kila leo huko Palestina.

Tags