May 19, 2022 12:27 UTC
  • Syria: Kuwepo haramu na kinyume cha sheria kwa Marekani katika ardhi yetu kunakaribia ukingoni

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema kuwepo haramu na kinyume cha sheria kwa Marekani mashariki ya nchi hiyo kunakaribia ukingoni.

Askari wa jeshi la kigaidi la Marekani na vibaraka wao wanaikalia kwa mabavu sehemu kubwa ya eneo la mashariki na kaskazini mashariki mwa Syria. Maeneo hayo ndiko iliko akiba kubwa ya rasilimali ya mafuta ya nchi hiyo.

Akizungumza katika mahojiano na chaneli ya As-Syria, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal al-Miqdad amesisitiza kuwa, maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yatarudi kwenye udhibiti wa serikali ya Syria; na wapiganaji wa Vikosi vya Kidemokrasia vya Wakurdi wa Syria wajue kwamba Wamarekani wavamizi wataondoka katika ardhi ya Syria na wao hawatakuwa na wa kumtegemea.

Askari wa jeshi la kigaidi la Marekani wakipora mafuta ya Syria katika maeneo wanayoyakalia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ameeleza kuwa vipaumbele vya sera za nchi hiyo viko thabiti na akaongeza kuwa, wakati maadui wa Syria walipoona wameshindwa kuidhoofisha Syria ili kuilazimisha ibadilishe misimamo yake waliamua kutumia mbinu ya vita vya kigaidi dhidi yake.

Halikadhalika, Faisal al-Miqdad ameutaka Umoja wa Mataifa  na nchi za dunia kuyatalii matukio ya Syria kwa kina na kwa insafu na sambamba na kushirikiana na serikali ya Damascus, kuunga mkono pia jitihada inazofanya za kuinua na kuimarisha muelekeo chanya na athirifu wa kisiasa ili kuleta maelewano nchini.../