May 20, 2022 01:21 UTC
  • Mamlaka ya Ndani ya Palestina yaionya Israel kwa hujuma zake dhidi ya msikiti wa al-Aqswa

Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeonya kuhusiana na matokeo mabaya ya vitendo vya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel vya kufanya hujuma na uvamizi dhidi ya msikiti wa al-Aqswa na kambi ya wakimbizi ya Jenin.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina  imeeleza kwamba, siasa za kivamizi za utawala bandia wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina zitapelekea kulipuka hali ya mambo katika ardhi za Palestina.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeashiria hujuma, uvamizi, jinai na kamatakamata inayofanywa na wanajeshi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika msikiti wa al-Aqswa na kambi ya wakimbizi ya Jenin na kubainisha kwamba, hatua hizo zitakuwa na matokeo mabaya.

Kuanzia mwezi uliopita wa Aprili mji wa Baytul-Muqaddas, msikiti wa al-Aqswa na kambi ya wakimbizi ya Jenin yameshuhudia kushadidi hujuma na mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Walowezi wa Kizayuni wakiuvamia msikiti wa al-Aqswa

 

Hatua hizo za kinyama zinakwenda sambamba na kasi ya ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

Wapalestina kwa upande wao wanasisitiza kuwa, muqawama na mapambano ya silaha ndio njia pekee ya kukabiliana na jinai za kila uchao za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Msimamo wa makundi ya mapambano ya Palestina ni kuwa, muqawama dhidi yaa adui Mzayuni utaendelea hadi pale ardhi yote ya Palestina itakapokombolewa na kutobakia hata kipande kidogo cha ardhi hiyo katika makucha ya Wazayuni maghasibu.

Tags