May 20, 2022 09:08 UTC
  • Tathmini ya uchaguzi wa Lebanon kwa mtazamo wa Sayyid Hassan Nasrullah

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa chama cha Hizbullah cha nchini Lebanon, juzi usiku alitoa hutuba akibainisha tathmini yake kuhusu matokeo ya uchaguzi wa hivi karibu wa bunge la nchi hiyo.

Huku zikiwa zimepita siku tano tu tangu uchaguzi wa bunge la Lebanon ufanyike, chambuzi na tathmini mbali mbali zimekuwa zikitolewa kuhusu matokeo ya uchaguzi huo. Baadhi ya watu wanazungumzia kushindwa Hizbullah na washirika wake katika uchaguzi huo, huku wengine wakiamini kuwa uchaguzi huo umeimarisha hali ya upinzani nchini Lebanon. Wale wanaoamini kushindwa Hizbullah katika uchaguzi huo wanaashiria kupoteza Hizbullah wingi mutlaki wa viti bungeni kwa kupungua viti hivyo kutoka viti 71 hadi 62, huku wakifumbia macho masuala matatu muhimu.

La kwanza ni kuwa idadi ya watu walioipigia kura Hizbullah na washirika wake katika uchaguzi huu mpya imeongezeka pakubwa. Pili, Hizbullah na washirika wake wanashikilia viti vingi zaidi bungeni. Tatu, idadi ya viti vya Hizbullah na Amal katika bunge jipya imeongezeka kutoka 28 hadi 31.

Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah

Ni wazi kuwa mtazamo huo wa uchambuzi ni mwendelezo wa mashinikizo na vita vya kisaikolojia ambavyo vimekuwa vikiendeshwa kwa muda mrefu dhidi ya Hizbullah. Kuhusiana na hilo, Sayyid Hassan Nasrullah alisema katika hotuba yake ya juzi usiku kwamba: "Licha ya miaka mingi ya kampeni za uchochezi dhidi ya mrengo wa mapambano zinazoongozwa na Wamarekani, ukweli ambao ameukiri wazi pia David Shanker, Naibu wa zamani wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika Masuala ya Mashariki ya Karibu, idadi ya kura na wabunge wetu imeongezeka."

Nukta nyingine ni kwamba kwa kawaida idadi ya wabunge walio wengi na walio wachache katika bunge la Lebanon hutathminiwa kwa mitazamo tofauti. Kimsingi, muundo wa mamlaka nchini Lebanon ni wa makubaliano, na uchaguzi wa viongozi hauwezi kutimia bila kutilia maanani maoni ya makundi mengine pinzani. Sayyid Hassan Nasrullah, akiwa na ufahamu kamili wa hali hiyo ya Lebanon, anajaribu kadiri anavyoweza kuyashawishi makundi mengine yazingatie umoja na maslahi ya kitaifa badala ya ukabila, huku akipinga madai kwamba mrengo wa mapambano ulishindwa katika uchaguzi wa karibuni.

Ni kwa msingi huo ndipo katika hotuba yake ya karibuni, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon akasema: "Hakuna kundi la kisiasa nchini ambalo linaweza kudai kuwa na wingi wa wabunge. Kufikia sasa, hakuna mtu yeyote aliye na heshima na busara ambaye ametoa madai kama hayo. Leo sisi tuna makundi na mirengo mingi ya wabunge, vyama vya siasa na wawakilishi wapya huru, ambapo huenda jambo hili likawa na maslahi kwa Lebanon na watu wa taifa hili ambapo hakuna kundi lolote linaloweza kudai kuwa na wingi wa kura bungeni." Kwa hakika kwa matamshi yake hayo, Sayyid Hassan Nasrullah kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa Lebanon ni taifa lenye makundi mengi ya kisiasa na kijamii.

Nukta ya tatu ni kuwa, matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni wa bunge la Lebanon ni ishara ya wazi ya kushindwa wapinzani wa mrengo wa mapambao hususan Saudi Arabia na Marekani, ambazo zimetumia gharama kubwa ya fedha kwa ajili ya kuyafanya makundi yanayoupinga mrengo huo yaweze kupata wingi wa kura katika bunge la Lebanon. Suala hili pia liliashiriwa katika hotuba ya hivi karibuni ya Sayyid Hassan Nasrullah. Huku akisisitiza kuwa madai ya Iran kuingilia masuala ya Lebanon ni uongo mtupu, Sayyid Hassan Nasrullah amesema: "Tulimwona balozi wa Marekani akipiga doria katika vituo vya kupigia kura na ubalozi wa Marekani ukitoa orodha. Tulimwona pia balozi wa Saudi Arabia akifanya kampeni kubwa zaidi za uchaguzi nchini Lebanon."

Bunge la Lebanon

Nukta ya mwisho ni kwamba wasi wasi mkuu wa Katibu Mkuu wa Hizbullah nchini Lebanon ni kuona kwamba nchi hiyo inatatua kwa mafanikio matatizo mengi sugu yanayoikabili. Baada ya kutangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa wabunge, Sayyid Hassan Nasrullah kwa mara nyingine amesisitiza haja ya kuwekwa kando tofauti na kuhitimishwa kampeni za uchaguzi ili kushughulikia matatizo na njia za kuboresha maisha ya wananchi wa Lebanon. Amesisitiza hilo kwa kusema: "Migogoro inaweza tu kutatuliwa kwa ushiriki na ushirikiano, mbali kabisa na uhasama. Kwa hivyo tunapasa kuzingatia yale yanayotuunganisha badala ya yale yanayotutenganisha."

Tags