May 21, 2022 10:28 UTC
  • Mwaka mmoja baada ya Vita vya Seif al-Quds

Mwaka mmoja umepita tangu kutokea Vita vya Seif al-Quds. Licha ya kupita mwaka mmoja tangu kumalizika vita hivyo, lakini natija ya vita hivyo haijaishia katika siku 12 tu za vita hivyo.

Vita vya Seif al-Quds vilianza Mei 10 mwaka jana 2021 na kufikia tamati baada ya siku kumi mbili. Mwaka mmoja umepita huku anga ya kisiasa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na Palestina sambamba na mizozo na mivutano baina ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Palestina imeshuhudia mabadiliko.

Katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina la Israel, Benjamin Netanyahu ambaye alianzisha vita dhidi ya Palestina kwa ajili ya kuhakikisha kuwa anabakia madarakani, aligaragazwa na kuondolewa madarakani na hivyo kuwekwa kando katika ulingo wa siasa za Israel baada ya kuweko katika uga huo wa kisiasa kwa miaka 12. Weledi wa mambo wanasema kuwa, kushindwa Israel katika Vita vya Seif al-Quds ilikuwa moja ya sababu kuu za kufanikiwa mahasimu wa kisiasa wa Netanyahu kumvua cheo cha Uwaziri Mkuu.

Baada ya kuondolewa madarakani Netanyahu, Bunge la utawala wa Kizayuni wa Iisrael likashuhudia kuingia madarakani Baraza la Mawaziri ambalo sifa yake muhimu ni kulegalega na kutokuwa imara na madhubuti.

Naftali Bennett alichukua jukumu la Uwaziri Mkuu ambapo ndani ya serikali hiyo walikuwemo wawakilishi vyama vya mrengo wa kushoto, mrengo wenye misimamo ya wastani na Waarabu huku Bennett mwenyewe akiwa ni kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia chenye misimamo mikali cha Yamina. Ni mara chache mno kushuhudiwa Baraza la Mawaziri huko Israel lenye mchanganyiko mkubwa wa mirengo mbalimbali huku likiwa limejaa watu na shakhsia wenye mitazamo kinzani kama la mara hii.

Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

 

Katika upande mwingine, cheo cha Waziri Mkuu ni cha mzunguko na mpokezano baina ya Yair Lapid na Naftali Bennett. Kwa sasa Bennett ndiye Waziri Mkuu wa Israel huku Yair Lapid ambaye filihali ni Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala huo ghasibu anatarajiwa kupokea wadhifa wa Uwaziri Mkuu kutoka kwa Bennett Novemba hapo mwaka 2023.

Kujiuzulu Idit Silman tarehe 6 Aprili mwaka huu kutoka katika muungano uliounda Baraza la Mawaziri kuliamsha cheche za matumaini kwa wapinzani kwa ajili ya kuiangusha serikali hiyo ya muungano. Serikali ya Bennett na Lapid ilifanikiwa kuundwa ikiongoza kwa zaidi ya kura moja tu yaani kura 61; na hivyo kujiuzulu Idit Silman kumeifanya serikali hiyo ipoteze uuungaji mkono wa waliowengi katika Bunge la Israel na kwa muktadha huo, viti vya Bunge vimegawanyika sawa kwa sawa yaani 60 kwa 60 baina ya muungano tawala na wapinzani.  

Fauka ya hayo, kujiuzulu Silman kulipokewa kwa mikono miwili na Benjamin Netanyahu ambaye ametupwa nje ya ulingo wa siasa za Israel. Netanyahu akiwa na wafuasi wake, walifanya mkusanyiko na kutangaza upinzani wao dhidi ya serikali ya sasa ya Bennet na Lapid na kutabiri kwamba, muda si mrefu serikali hiyo ya muungano itasambaratika. Wiki mbili baada ya kujiuzulu Idit Silman, orodha ya pamoja ya Waarabu ambayo ni sehemu ya muungano unaotawalaiumeanza kutoa matamashi ya chini kwa chini kuhusianan na kutaka kujiondoa katika muungano huo.

Mwaka mmoja tangu kutokea Vita vya Seif al-Quds hali ya serikali ya mpokezano wa madaraka huko Israel imezidi kutetereka zaidi. Nukta muhimu ni hii kwamba, Wapalestina wana mchango mkubwa wa hali inayowakumba Bennet na mshirika wake Yair Lapid katika serikali ya sasa.

Wanamapambano wa HAMAS

 

Serikali hii kama iilivyokuwa ile ya Benjamin Netanyahu, imeliweka katika ajenda zake suala la kuwakandamiza Wapalestina na hata vitendo hivyo vya ukandamizaji vinaonekana kuchukua mkondo na wigo mpana zaidi. Hii leo tunashuhudia operesheni za kujitolea kufa shahidi Wapalestina katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel. Hadi sasa kumetekelezwa operesheni 5 za kujitolea kufa shahidi katika kipindi cha miezi miwili na kupelekea Wazayuni 19 kuangamizwa na kujeruhiwa.

Mwaka mmoja baada ya Vita vya Seif al-Quds imedhihirika wazi kuweko pigo la kiintelijensia na kiusalama dhidi ya utawala huo ghasibu katika ardhi unazozikalia kwa mabavu na viongozi wa utawala huo wamechanganyikiwa na kushindwa la kufanya kuhusiana na fedheha hii.

Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ukiwa na lengo la kukabiliana na pigo na fedheha hii ya kiintelijensia na kiusalama umetoa vitisho vya kuwaua makamanda wa Kipalestina. Vitisho hivyo ni ithbati tosha kwamba, wasiwasi wa Naftali Bennett na Yair Lapid wa kusambaratika serikali yao umeongezeka maradufu hasa baada ya kushindwa kukabiliana na operesheni za kujitolea kufa shahidi za Wapalestina.

Kuhusiana na hilo, makundi ya muqawama Palestina yametoa taarifa ya pamoja na kutangaza kuwa, Upanga wa Quds ungali nje ya ala yake na kwamba, vitisho vya utawala vamizi wa Israel vya kuwaua viongozi wa muqawama ni ishara ya wazi ya kutokuwa na uwezo, kuchanganyikiwa na kushindwa utawala huo kukabiliana na wanamapambano wa Kipalestina. 

Tags