May 22, 2022 04:38 UTC
  • Jeshi la Yemen latungua droni nyingine ya kijasusi ya Saudia mkoani Hajjah

Msemaji wa majeshi ya Yemen ametangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kutungua droni - yaani ndege isiyo na rubani - ya kijasusi ya Saudi Arabia katika mkoa wa Hajjah.

Televisheni ya Almasirah imemnukuu Brigedia Jenerali Yahya Saree akitangaza habari hiyo na kusisitiza kuwa, Jeshi la Yemen limefanikiwa kutungua ndege moja ya kijasusi isiyo na rubani ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia wakati ilipokuwa inafanya ujasusi katika mkoa wa Hajjah.

Tangu Saudia ilipoongozwa uvamizi wa Yemen mwezi Machi 2015, Jeshi la Yemen kwa kushirikiana na vikosi vya ukombozi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo limesimama imara kuilinda Yemen na hadi hivi sasa limeshatungua mamia ya ndege za kijasusi zisizo na rubani za muungano huo vamizi.

Brigedia Jenerali Yahya Saree

 

Nguvu za Kijeshi za Yemen ni kubwa na zimevuruga njama zote za muungano vamizi licha ya nchi hiyo kuzingirwa kila upande, angani, ardhini na baharini na licha ya kufanyiwa ukatili mkubwa ambao ni mara chache umeripotiwa kwenye kumbukumbu za historia.

Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Yemen amesema, majeshi ya nchi hiyo yako macho na yataendelea kutoa majibu makali na ya haraka dhidi ya uvamizi wowote ule.

Mbali na Vikosi vya Ulinzi vya Yemen kufanikiwa kuilinda nchi hiyo, vimefanikiwa pia kutoa vipigo vizito kwa nchi vamizi hasa Saudi Arabia na kufelisha njama zao. Ikumbukwe kuwa mshirika mkubwa wa Saudia katika uvamizi wa Yemen ni Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati). Jeshi la Yemen limefanya mashambulio kadhaa huko Imarati na kuwatia woga mkubwa viongozi wa nchi hiyo inayotegemea mno usalama kuvutia wawekezaji.