May 22, 2022 07:59 UTC
  • Bunge la Iraq: Tumeazimia kuzuia kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel

Spika wa Bunge la Iraq amesisitiza kuwa, taasisi hiyo imeazimia kuzuia kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Mohammed al-Halbousi, Spika wa Bunge la Iraq ameeleza kwamba, hatua za utawala wa muda wa Israel kuanzia jinai zake mpaka kupuuza waziwazi thamani na misingi ya ubinadamu ni mambo ambayo yanaweka wazi sura halisi ya utawala huo ghasibu.

Mohammed al-Halbousi ameongeza kuwa, tangu miongo kadhaa nyuma kadhia ya Palestina imekuwa miongoni mwa mambo ya awali na yanayopewa kipaumbele na wananchi wa Iraq na kubainisha kwamba, hali ya Quds na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hususan matukufu ya Kiislamu na Kikristo, ni mambo ambayo yanalazimu mataifa ya Kiarabu kuchukua msimamo mmoja hatua ambayo itakuwa chachu ya kuchukuliwa msimamo wa wazi wa kimataifa.

Maandamano ya kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel

 

Hivi karibuni, Bunge la Iraq liliidhinisha rasimu ya sheria inayopiga marufuku kuanzisha au kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Rasimu hiyo inatoa adhabu ya kifo kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kuhusika na uhalifu huo.

Nchi za Kiarabu zilianza kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa kibaguzi wa Israel tangu Septemba 2020 kwa upatanishi au hata kwa kulazimishwa na utawala wa Doland Trump, rais wa zamani wa Marekani.

Nchi nne za Imarati, Bahrain, Morocco na Sudan zilianzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu unaoendelea kuikaliwa kwa mabavu Quds Tukufu mwaka 2020, hatua ambayo imeendelea kulalamikiwa na Waislamu na wapenda haki.

Tags