May 22, 2022 10:54 UTC
  • Reuters: Makabidhiano ya madaraka yamekaribia nchini Saudi Arabia

Shirika la habari la Reuters limezinukuu duru za Saudi Arabia zikisema kuwa, hatua ya kuweko Abdul Aziz bin Ahmad katika msafara wa Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia alipotembelea Imarati hivi karibuni, ni ishara kwamba mchakato wa kukabidhiana madaraka umekaribia huko Saudia.

Afisa mmoja mwandamizi wa Saudi Arabia ameliambia shirika hilo la habari la Uingereza kuwa, baadhi ya matukio katika medani ya kisiasa huko Saudia yanaonesha kuwa, mchakato wa kukabidhiana madaraka kutoka kwa mfalme kwenda kwa mrithi wa ufalme umekaribia mno.

Televisheni ya al Alam imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, duru hiyo ya kuaminika ya Saudia, imegusia kuweko Abdul Aziz bin Ahmad katika msafara wa Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia katika ziara ya hivi karibuni ya kuutembelea Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati), na kusema, hiyo ni ishara ya wazi kuwa karibuni hivi ufalme wa Saudia utaingia rasmi mikononi mwa Mohammad bin Salman.

Mohammad bin Salman

 

Ikumbukwe kuwa mwanamfalme Ahmad bin Abdul Aziz mtoto mkubwa wa kiume wa Abdul Aziz bin Ahmad, ndugu wa mfalme Salman bin Abdul Aziz yuko jela hivi sasa kwa amri ya Mohammad bin Salman.

Kwa muda mrefu mfalme Salman bin Abdul Aziz ni mgonjwa na taarifa za hivi karibuni zinasema kuwa mfalme huyo alilazwa katika hospitali moja mjini Jeddah kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kitiba, wiki kadhaa tangu alipobadilishiwa betri ya kusaidia mapigo ya moyo.

Taarifa iliyotolewa na shirika rasmi la habari la Saudia, SPA haikutoa maelezo zaidi kuhusu hali ya afya ya mfalme huyo mzee mwenye umri wa miaka 86 wala aina ya uchunguzi na ukaguzi aliyofanyiwa katika hospitali ya utaalamu maalumu ya Mfalme Faisal.