May 22, 2022 10:58 UTC
  • Jihad al Islami: Muda mrefu sasa utawala wa Kizayuni haujaonja ushindi

Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa harakati ya Jihad al Islami ya Palestina amesema kuwa, tangu baada ya vita vya siku sita vya 1967, jeshi la utawala wa Kizayuni halijawahi tena kuonja ladha ya ushindi dhidi ya mataifa ya Waislamu na Waarabu.

Televisheni ya al Alam imemnukuu Walid al Qatati akisema hayo kwenye sherehe za mwaka wa kwanza wa operesheni ya Seif al Quds yaani Upanga wa Quds na huku akikumbushia ukombozi wa maeneo ya kusini mwa Lebanon na Ukanda wa Ghaza amesisitiza kuwa, kumbukumbu ya opereseheni ya Upanga wa Guds ndio mwanzo wa kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu.

Operesheni ya Seif al Quds au Upanga wa Quds ni vita vya pande zote vilivyoendeshwa na makundi ya muqawama ya Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni na ambavyo vilianza tarehe 11 Mei 2021 na kuendelea kwa muda wa siku 12. 

Nembo ya harakati ya Jihad al Islami ya Palestina

 

Makundi ya mapambano ya Kiislamu ya Ukanda wa Ghaza hasa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Jihad al Islami ya Palestina ziliusababishia hasara kubwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita hivyo.

Ushindi huo wa makundi ya muqawama ya Palestina umekuwa ni mwiba kwenye jicho la utawala wa Kizayuni na tangu wakati huo hadi hivi sasa una kiwewe cha kuingia tena kwenye vita vikubwa na makundi ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina.

Walid al Qatati amesema, kubanwa vibaya na kuchezeo kipigo Israel kumesababisha mgogoro wa uwepo wa utawala huo pandikizi na jambo hilo ni udhibitisho kuwa wakati wa kusambaratika utawala wa Kizayuni wa Israel na kufutika kabisa katika uso wa dunia, unazidi kukaribia.