May 23, 2022 03:44 UTC
  • Watangazaji wanawake Afghanistan wafunika nyuso baada ya kukaidi agizo la Taliban kwa siku moja

Watangazaji wanawake wa televisheni nchini Afghanistan wameridhia kutangaza wakiwa wamefunika nyuso zao kulingana na agizo lililotolewa na serikali ya Taliban, baada ya kukaidi kufanya hivyo kwa muda wa siku moja.

Siku ya Jumamosi, na baada ya kutolewa agizo la serikali ya Taliban la kuwaamuru watangazaji wote wanawake wa televisheni wafunike kikamilifu nyuso zao wakati wanapotangaza, rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai aliwataka watangazaji hao wakaidi agizo hilo. Wanawake hao walifanya hivyo na kuingia studio za chaneli za televisheni kutangaza bila kufunika sura zao.

Hata hivyo jana Jumapili, watangazaji hao walitekeleza agizo hilo la Taliban kwa kufunga kitambaa kinachobakisha wazi macho na kipaji cha uso badala ya kizoro aina ya burqa kinachofunika sura yote.

Ripoti kutoka mji mkuu wa Afghanistan, Kabul zinaeleza kuwa, jana Jumapili, watangazaji wanawake wa televisheni ya Tolue News, televisheni ya Aryana na Shamshad tv waliingia studio kutangaza wakiwa wamefunika nyuso zao. 

Haibatullah Akhunzada

Sonia Niyazi, mtangazaji wa televisheni ya Tolue News amevieleza vyombo vya habari: "Sisi tumekataa na tumepinga kuvaa burqa. Hata hivyo Taliban imeishinikiza Tolue News na kuieleza kwamba watangazaji wanawake wanaotaka kutangza bila kufunika nyuso zao itabidi wabadilishe aina ya kazi wanazofanya".

Mnamo takriban wiki tatu nyuma, Kiongozi Mkuu wa Taliban nchini Afghanistan Haibatullah Akhunzada alitoa agizo lenye vipengee vinne la sheria mpya kuhusu mipaka ya vazi la Hijabu kwa wanawake wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa agizo hilo, wanawake wote wanalazimika kuvaa hijabu, ikiwemo kufunika nyuso zao wanapokuwa katika hadhara na kwamba watakaohalifu kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali.

Kupitia wizara yake ya kuamrisha mema na kukataza maovu, serikali ya Taliban ilisisitiza katika agizo kwamba, wanawake wasiovaa hijabu ambao wanafanya kazi katika idara za serikali wataachishwa kazi.../

Tags