May 24, 2022 11:10 UTC
  • Jeshi la Yemen latungua ndege ya kivita ya Saudia katika anga ya Sana'a

Muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia umerusha ndege ya kivita isiyo na rubani katika anga ya mji mkuu wa Yemen, Sana'a kwa lengo la kutekeleza oparesheni za kichokozi lakini Jeshi la Yemen limefanikiwa kuitambua ndege hiyo vamizi ya adui na kuitungua papo hapo.

Uchokozi huo wa Saudia unakuja pamoja na kuwa kuna mapatano ya usitishwaji vita Yemen yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa na yaliyoanza kutekelezwa mwanzoni mwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigeida Jenerali Yahya Saree ametuma ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter na kusema, vikosi vya ulinzi wa anga vya Yemen vimefanikiwa kuitungua ndege ya kivita ya Saudia isiyo na rubani aina ya CH-4 iliyoundwa China. Amesema ndege hiyo vamizi ya Saudia imetunguliwa kwa kombora la nchi kavu kuelekea angani wakati ikitekeleza oparesheni za kiuadui katika anga ya Sana'a Jumatatu usiku.

Ndege isiyo na rubani ya CH-4 ina uwezo wa kuruka hadi umbali wa kilomita 5,000 na ina uwezo wa kubebe hadi makombora sita.

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigeida Jenerali Yahya Saree

Tukio hilo limekuja siku mbili tu baada ya Majeshi ya Yemen kutungua ndege nyingine ya kivita isiyo na rubani ya muungano wa kivita wa Saudia aina ya Karayel iliyoundwa Uturuki. Ndege hiyo vamizi ilitunugliwa wakati ikiendeleza oparesheni za kivita katika anga ya wilaya ya Hayran.

Tangu Saudia ilipoongoza uvamizi wa Yemen mwezi Machi 2015, Jeshi la Yemen kwa kushirikiana na vikosi vya ukombozi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo limesimama imara kuilinda Yemen na hadi sasa limeshatungua mamia ya ndege za kijasusi zisizo na rubani za muungano huo vamizi.