May 25, 2022 02:30 UTC
  • HAMAS yawataka Wapalestina kujitokeza kwa wingi kuutetea Msikiti wa al-Aqswa

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amewatolea wito Wapalestina wote kujitokeza kwa wingi katika msikiti wa al-Aqswa kwa ajili ya kulitetea eneo hilo takatifu.

Muhammad Hamada, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amewataka Wapalestina kujitokeza kwa wingi Jumapili ijayo katika msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kwa ajili ya kukabiliana na walowezi wa Kizayuni ambao wamekuwa wakiuvamia na kuuhujumu msikiti huo.

Kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa HAMAS ameeleza kuwa, ni jukumu la Wapalestina kujitokeza katika Masjidul al-Aqswa kwa ajili ya kusambaratisha njama  na mipango michafu ya adui Mzayuni na walowezi wa Kizayuni.

Kadhalika msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amebainisha kwamba, himaya ya Wapalestina kwa msikiti wa al-Aqswa ni ujumbe unaofahamisha maadui kwamba, msikiti huo mtakatifu ni mstari mwekundu kwa Wapalestina na kwamba, wavamizi hawana nafasi yoyote katika msikiti huo.

Walowezi wa Kizayuni wakiingia katika Msikiti wa al-Asqswa

 

Kuanzia mwezi uliopita wa Aprili mji wa Baytul-Muqaddas, msikiti wa al-Aqswa na kambi ya wakimbizi ya Jenin yameshuhudia kushadidi hujuma na mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Hatua hizo za kinyama zinakwenda sambamba na kasi ya ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

Wapalestina kwa upande wao wanasisitiza kuwa, muqawama na mapambano ya silaha ndio njia pekee ya kukabiliana na jinai za kila uchao za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina.