May 25, 2022 07:24 UTC
  • Jeshi la Yemen latungua ndege ya tatu ya kijasusi ya Saudi Arabia

Jeshi la Yemen limetangaza kuwa limefanikiwa kutungua droni yaani ndege isiyo na rubani ya Saudi Arabia katika eneo la kaskazini magharibi mwa Yemen.

Televisheni ya al Alam imenukuu taarifa ya Brigedia Jenerali Yahya Saree aliyoandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Jumanne na kusema kuwa, kikosi cha ulinzi wa anga cha Yemen kimefanikiwa kutungua ndege ya kijausi ya Saudia wakati ilipokuwa inafanya ujasusi na operesheni ya kiuadui katika eneo la mpakani la Najran. Amesema, uchokozi huo wa Saudi Arabia ni uvunjaji wa wazi wa makubaliano ya kusimamisha vita yalivyofikiwa miezi miwili iliyopita.

Amesema, ndege hiyo ya kijasusi ya Saudia imetunguliwa na kikosi cha ulinzi wa anga cha Yemen kwa kutumia kombora lililotengenezwa ndani ya Yemen. Amesema karibuni hivi jeshi hilo litasambaza picha na video zinazoonesha operesheni ya kutunguliwa ndege hiyo ya kijasusi ya Saudi Arabia.

Brigedia Jenerali Yahya Saree

Mapema jana asubuhi pia, jeshi la Yemen lilitungua ndege ya kijasusi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia katika anga ya mji mkuu Sana'a. Ndege ya kijasusi iliyotunguliwa Sanaa, ilikuwa imetengenezwa China. Juzi pia jeshi hilo lilitungua ndege nyingine ya wavamizi hao katika anga ya Yemen. Hii ina maana kuwa ndege ya kijasusi ya Saudia iliyotunguliwa huko Najran ni ya tatu katika kipindi cha siku mbili.

Muda wa makubaliano ya kusimamisha vita yaliyopendekezwa na Umoja wa Mataifa unamalizika siku tisa zijazo kati ya wavamizi wa Yemen na jeshi na vikosi vya kujitolea vya ukombozi wa nchi hiyo. Ijapokuwa kuna uwezekano wa kuongezwa muda wa usimamishaji vita huo, lakini Saudia imeshadidisha uvunjaji wake wa makubaliano ya hivi sasa yalivyoanza kutekelezwa miezi miwili nyuma.