May 25, 2022 10:53 UTC
  • Uturuki yazidi kustawisha uhusiano na Israel, waziri wake wa mambo ya nje awasili Tel Aviv

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amewasili uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Cavusoglu, amefanya safari hiyo leo licha ya viongozi wa serikali ya Uturuki inayoongozwa na Recep Tayyip Erdoğan kutangaza mara kadhaa kuwa Ankara inawahami na kuwaunga mkono wananchi wa Palestina katika kukabiliana na ukaliaji kwa mabavu wa ardhi zao na jinai zinazofanywa na utawala haramu wa Kizayuni dhidi yao.

Hata hivyo uungaji mkono huo umeonekana kuwa ni wa maneno matupu kutokana na Uturuki na utawala bandia wa Israel kuendelea kufanya mazungumzo ya siri katika nyanja zote. Mapema mwezi Machi mwaka huu, rais Isaac Herzog wa utawala wa Kizayuni alitembelea Uturuki kwa mwaliko rasmi wa Erdoğan, ziara ambayo ilipingwa na kulalamikiwa na wananchi wa Uturuki.

Erdogan (kulia) na Herzog walipokutana mjini Ankara

Uturuki iliutambua utawala wa Kizayuni mwaka 1949, na kuanzia wakati huo pande hizo mbili ziliasisi uhusiano wa karibu katika nyuga za kiuchumi na kijeshi.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amewasili uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na kulakiwa na maafisa wa kidiplomasia wa utawala huo. Hiyo ni safari ya kwanza kufanywa na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Israel baada ya miaka 15.

Cavusoglu amekutana na kufanya mazungumzo na waziri mwenzake wa utawala wa Kizayuni Yair Lapid.

Taha Ozhan, mwenyekiti wa zamani wa kamati ya mambo ya nje katika bunge la Uturuki amesema, lengo la nchi hiyo na Israel wakati huu ni kurejesha tena uhusiano madhubuti wa kidiplomasia baina yao na kuona kama itawezekana kufanya kazi pamoja hapo baadaye katika baadhi ya maeneo.../

 

Tags