May 26, 2022 03:53 UTC
  • Indhari ya Antonio Guterres kuhusu ukimbizi; Asia Magharibi kitovu cha mgogoro

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekosoa vikali mwenendo wa kulazimika watu wa mataifa mbalimbali kuyakimbia makazi yao na kuutaja ukimbizi kuwa ni mgogoro wa kisiasa.

Guterres ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: "Filihali watu milioni 100 wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kuishi maisha ya ukimbizi. Huu sio mgogoro wa ukimbizi, na wakimbizi sio wasababishaji wa jambo hili. Huu ni mgogoro wa kisiasa na unaweza kupatiwa ufumbuzi tu kwa kuweko mshikamano na irada ya kisiasa."

Mgogoro wa ukimbizi hususan katika muongo wa pili wa karne ya 21 ulichukua mkondo na wigo mpana zaidi sambamba na kuibuka migogoro katika eneo la Asia Magharibi. Wachambuzi wa mambo wanalitaja wimbi kubwa la wakimbizi kwa majina mbalimbali kama "Uhajiri Mkubwa" au Janga la Kimyakimya" ambalo lilianza katika muongo wa pili wa karne ya 21 na lingali linashuhudiwa hadi sasa.

Harakati za makundi yenye misimamo ya kufurutu ada yanayoungwa mkono na madola ya Magharibi na baadhi ya madola ya eneo ni mambo yaliyoandaa uwanja na mazingira ya kuibuka machafuko ya ndani na vilevile vita vya kigaidi. Magaidi wakiungwa mkono na madola ya Magharibi na washirika wao, wamefanya mauaji na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya raia hususan wanawake na watoto. Ukatili huu ambao haujawahi kushuhudiwa imeifanya sehemu kubwa ya wahanga wa vitendo hivi kuwa wakimbizi.

Syria na Iraq ni mataifa mawili ya Asia Magharibi ambayo yameshuhudia ukatili na utumiaji mabavu mkubwa kuliko nchi nyingine yoyote katika eneo hili ambapo natija yake ni mamilioni ya raia wa nchi hizi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi zao.

Wakimbizi wa Ukraine

 

Yemen ni nchi nyingine ambayo imekuwa na wakimbizi wengi katika miaka ya hivi karibuni. Vita visivyo na mlingano vya utawala vamizi wa Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen ambavyo vimesababisha kusambaratika miundombinu na kuuawa na kujeruhiwa maelfu ya raia, ni chimbuko la kuwa wakimbizi nchini Yemen hususan wanawake na watoto.

Pamoja na hayo, wananchi wa Yemen kabla ya kukimbilia nje ya nchi wamelazimika kuwa wakimbizi ndani ya taifa lao ambapo hali hii nayo imekuwa na taathira mbaya kwao hususan njaa na magonjwa mbalimbali kama kipindupindu na kadhalika.

Kuna kipindi Palestina ilikuwa ndio taifa lenye wakimbizi wengi zaidi duniani. Licha ya kuwa, rekodi hiyo sasa inashikiliwa na mataifa mengine ikiwemo Syria, lakini wakimbizi wa Palestina wangali wanataabika katika maisha yao ya ukimbizini wakiwa katika mataifa mbalimbali. Utawala haramu wa Israel umekuwa ukiwazuia Wapalestina hao kurejea katika nchi yao.

Kuanguka serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani nchini Afghanistan na kundi la wanamgambo wa Taliban kudhibiti mamlaka ya nchi, ni jambo ambalo liliwaaacha midomo wazi walimwengu wote. Picha na taswira zilizokuwa zikihusiana na wimbi la wahajiri na kuondoka raia wa Afghanistan katika Uwanja wa Ndege wa Kabul zilikuwa ni za kusikitisha mno. Kwa mara nyingine tena mamilioni ya Waafghani wakawa wakimbizi na mgogoro wa wakimbizi ukawa unagonga vichwa vya habari.

Msururu mrefu wa wakimbizi Ulaya Mashariki

 

Nukta nyingine muhimu ni namna ya uondokaji wa wakimbizi katika nchi zao. Wakimbizi ambao  katika hali ambayo wamelazimika kuondoka katika nchi zao na kuelekea katika mataifa mengine, hawakutumia njia salama na za kisheria, kwani kivitendo hakukuweko na uwezekano wa kutumia njia hizo. Namna ya uondokaji wa wakimbizi wa Kiafghani umeakisiwa mara chungu nzima katika vyombo vyya habari na kubainisha hofu na wasiwasi mkubwa wa wananchi hao wa kuingia madarakkani kundi la Taliban nchini Afghanistan.

Ni kwa msingi huo, ndio maana Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akaandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: " Sisi tunahitajia njia salama na za kisheria kwa ajili ya wahajiri na wakimbizi."

Kuibuka mgogoro wa Ukraine nako kwa mara nyingine tena kumekuwa chimbuko la kuzingatiwa suala la wakimbizi. Tofauti ya mgogoro wa Ukraine na wa mataifa ya eneo la Asia Magharibi ni kuwa, mgogoro wa wakimbizi wa Asia Magharibi umepuuzwa kikamilifu na madola ya Magharibi, huku hali ikiwa tofauti kabisa kuhusiana na wakimbizi wa Ukraine ambao wanazingatiwa na kupewa umuhimu sambamba na kufanyika juhudi maradufu za kuwasaidia.

Nukta ya mwisho ni kuwa, hivi sasa pia kama hakutakuweko na irada na azma ya kilimwengu ya kushughulikia mgogoro wa wakimbizi, hali ya mambo itakuwa mbaya zaidi na kutatokea maafa makubwa zaidi katika mustakabali.

Tags