May 27, 2022 09:10 UTC
  • Utawala wa Kizayuni wa Israel, utawala wa mauaji

Gazeti la Marekani la New York Times limeripoti kuwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umeitaarifu Marekani kwamba ndio uliohusika na mauaji ya Shahidi Hassan Sayyad Khodaei.

New York Times limezinukuu duru za kuaminika na kuandika kuwa, msemaji wa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni amekataa kueleza chochote kuhusu mauaji hayo, lakini kwa mujibu wa afisa mmoja wa intelijensia, utawala wa Kizayuni umewapa taarifa viongozi wa Marekani kwamba mauaji ya Shahidi Khodaei yamefanywa na maajenti wa utawala huo dhalimu.

Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ni kambi ya maandalizi na malezi ya magaidi. Kuandaa magaidi ni dhati ya utawala haramu wa Israel na tunaweza kusema kwamba mauaji, ndiyo yaliyokuwa na nafasi kuu na ya msingi katika kuasisiwa utawala huo wa Wazayuni. Viongozi wengi wa Palestina na Lebanon wameuliwa na utawala wa Kizayuni; na hata hivi karibuni, maafisa wa Kizayuni wametishia kwamba watamuua Yahya Al-Sinwari, kiongozi wa harakati ya Hamas katika Ukanda wa Gaza. 

Mbali na viongozi wa Palestina na Lebanon, wanasayansi wengi, hususan wanasayansi wa Iran na pia waandishi wengi wa habari wameuliwa na utawala wa Kizayuni; wa karibuni zaidi ni Shireen Abu Akleh, mwandishi wa habari Mpalestina wa televisheni ya Aljazeera ya Qatar, ambaye aliuliwa hivi karibuni na askari wa Israel wakati alipokuwa akiripoti habari huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Tangu mwaka 2000 hadi sasa, waandishi wa habari wasiopungua 45 wameuliwa na utawala haramu wa Kizayuni.

Hakuna shaka kuwa, mauaji ya Shahidi Sayyad Khodaei, Mlinzi wa Haram, ambaye ametoa mchango mkubwa katika kupambana na ugaidi nchini Syria, hayatakuwa ya mwisho kufanywa na maajenti wa utawala haramu wa Israel. Kuchukua utawala wa Kizayuni hatua ya kufanya mauaji mbalimbali kunachangiwa zaidi na mambo mawili. La kwanza ni kwamba, mauaji ndio yaliyowawezesha Wazayuni kufanya uvamizi na kukalia ardhi kwa mabavu. Na jambo la pili ni kuwa, mauaji ni matunda na matokeo ya uungaji mkono wa kila hali wa madola ya Magharibi na hasa Marekani kwa utawala wa Kizayuni. Na ithibati ya uungaji mkono huo, ni hatua ya viongozi wa Kizayuni kuitaarifu serikali ya Marekani kwamba wamemuua Shahidi Sayyad Khodaei.  

Kushoto: Shahidi Hassan Sayyad Khodaei. Kulia: eneo la tukio aliposhambuliwa ndani ya gari mbele ya nyumba yake

Kupewa taarifa hiyo maana yake ni kwamba serikali ya Marekani inaunga mkono jinai na uhalifu unaofanywa na utawala wa kigaidi wa Kizayuni. Saeed Khatibzadeh, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "jinai hii ya kinyama imefanywa na maajenti wa kigaidi ambao ni vibaraka wa Uistikbari wa dunia hali ya kuwa, kwa masikitiko makubwa, imeungwa mkono na kunyamaziwa na nchi zinazojinasibu kuwa zinapambana na ugaidi."

Lakini mbali ya hayo, kabla ya mauaji ya Shahidi Khodaei, waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni Benny Gantz alielekea Marekani, ambako alikutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa usalama na intelijensia wa nchi hiyo. Katika safari hiyo, Gantz alitoa matamshi mengi ya porojo dhidi ya Iran; na inavyoonekana, aliwataarifu viongozi wa Marekani kuhusu mpango wa mauaji ya Kanali Khodaei hata kabla hayajafanywa.

Suali la msingi la kujiuliza ni, kwa nini utawala wa Kizayuni umemuua Shahidi Sayyad Khodaei? Hata kama Wazayuni wametoa madai kadhaa kama kusema kwamba Shahidi Khodaei alikuwa akihusika na kuipatia Hizbullah ya Lebabon teknolojia ya makombora ya kisasa na yenye shabaha kali au kwamba Kanali Khodaei ndiye mpangaji wa operesheni eti za kigaidi dhidi ya Wazayuni, lakini ukweli wa kadhia hiyo ni kitu kingine kabisa.

Kwa upande mmoja, katika siku za karibuni na baada ya safari za Enrique Mora, mkuu wa timu ya mazungumzo ya Umoja wa Ulaya na ya Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani hapa mjini Tehran, zilijitokeza dalili za kufufuliwa mazungumzo ya Vienna. jambo ambalo kwa mtazamo wa Wazayuni, linagongana na maslahi yao na wanataka mazungumzo hayo yavunjike moja kwa moja.

 Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani (kulia) alipoonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei hapa Tehran

Lakini kwa upande mwingine, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa mwafaka katika mazungumzo utaweza kufikiwa kwa sharti kwamba Marekani iliondoe jina la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwenye orodha yake ya makundi ya kigaidi. Kuhusiana na suala hilo, katika ripoti yake, gazeti la New York Times limewanukuu baadhi ya wachambuzi na kuandika kuwa, utawala wa Kizayuni umefanya mauaji hayo kwa lengo la kuzuia Iran na Marekani zisifikie makubaliano katika mazungumzo ya nyuklia na jina la IRGC lisiondolewe kwenye orodha ya Washington ya makundi ya kigaidi.

Nukta nyingine ni kwamba, inavyoonyesha, mauaji ya Shahidi Khodaei yana uhusiano pia na mazoezi ya kijeshi yanayofanywa hivi sasa na utawala huo wa kigaidi wa Israel, kwani katika maneva hayo, utekelezaji wa jinai za mauaji umefanyiwa mazoezi pia.../

Tags