Jun 06, 2022 10:11 UTC
  • Ismail Hania asisitiza kuuhami Msikiti wa al-Aqswa kwa kutumia nyenzo zote

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesisitiza udharura wa kutumiwa suhula na nyenzo zote kwa ajili ya kuulinda na kuuhamai Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa.

Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema hayo katika mazungumzo yake na wajumbe wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu na kubainisha kwamba, kuna haja na ulazima wa kutumiwa nyenzo na suhula zote kwa ajili ya kuuhami msikiti wa al-Aqswa na utambulisho wake wa Kiislamu.

Hania ameashiria jinai za hivi karibuni za utawala ghasibu wa Israel katika Msikiti wa al-Aqswa na kufanyika huko Quds maandamano ya kichochezi yanayojulikana kama Maandamano ya Bendera na kusema kwamba, kuna ulazima wa kufanyika juhudi zote za kuuhami na kuutetea Msikiti wa al-Aqswa pamoja na utambulisho wake wa Kiislamu.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema pia kuwa, Quds na Msikiti wa al-Aqswa ni viini viwili vikuu vya umoja wa Umma wa Kiislamu.

Walowezi wa Kizayuni wakiingia katika msikiti wa al-Aqswa

 

Wakati huo huo, makundi mbalimbali ya Kipalestina yamewatolea wito Wapalestina kukusanyika mnamo siku zijazo katika msikiti wa Al Aqsa kukabiliana na njama nyingine ya walowezi wa kizayuni.

Katika kukabiliana na miito iliyotolewa kwa walowezi wa Kizayuni kushiriki kwenye hujuma nyingine ya kuuvamia msikiti wa al-Aqswa katika mkusanyiko uliopewa jina la "Sikukuu ya Majuma", makundi mbalimbali ya Kipalestina yametoa wito wa kuwataka Wapalestina wakusanyike katika miskiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

Tags