Jun 11, 2022 10:14 UTC
  • Hatua ya Israel kupora nishati ya Lebanon kwa mtazamo wa Sayyid Hassan Nasrallah

Sayyid Hassan Nasrallah, ametoa hutuba kuhusu hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupora utajiri wa nishati ya Lebanon ambapo amebainisha nukta kadhaa kuhusu kadhia hiyo.

Maudhui ya kuainisha mipaka ya baharini ni moja ya masuala ambayo Lebanon inahitilafiana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mnamo Oktoba 2020, Tel Aviv na Beirut, kwa upatanishi wa Marekani zilifanya mazungumzo ya kuainisha mipaka ya baharaini kwa lengo la kuanza uchimbaji gesi katika eneo hilo. Hata hivyo mazungumzo yalisitishwa mwezi Mei 2021 baada ya kushadidi hitilafu baina ya pande mbili kuhusu umiliki wa eneo linalozozaniwa baharini. Pamoja na kuwa mazungumzo yamesitishwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hivi karibuni umechukua hatua ya kichokozi na kuvuka mpaka wa baharini wa Lebanon na kuweka jukwaa la gesi katika Bahari ya Mediterania ukipanga kulitumia jukwaa hilo kuchimba mafuta na gesi katika eneo la machimbo ya gesi la Karish. Lebanon inasisitiza kuwa maadamu hakuna mapatano, utawala wa Israel hauna haki ya kuchimba gesi katika eneo hilo linazozaniwa na pande mbili. Ni kwa msingi huo ndipo Sayyid Hassan Nasrallah mnamo 9 Juni akatoa hotuba akifafanua kadhia hiyo.

Nukta ya kwanza katika hotuba ya Sayyid Hassan Nasrallah ni kuwa, machimbo ya gesi asilia ya Karish ni kati ya maeneo yanayozozaniwa baina ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo kuingia meli ya Ugiriki katika eneo hilo kwa lengo la kuchimba gesi ni uporoaji wa utajiri ambao bado kuna mzozo kuhusu umiliki wake. Sayyid Nasrallah amesema: "Meli hii imefika katika eneo kuchimba na kuzalisha gesi katika eneo ambalo linazozaniwa baina ya Lebanon na utawala ghasibu."

Nukta ya pili ni kuwa, Marekani na Israel zinataka kupora sehemu kubwa ya eneo la kijiografia la Lebanon. Hilo halishangazi kwani huu ndio utambulisho halisi wa utawala ghasibu wa Israel ambao umekuwa ukipora na kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na pia ardhi za Syria na Lebanon. 

Meli ya Shirika la Energean  ambayo imekodiwa na Israel ikiwa katika eneo lenye utajiri wa gesi baharini ambalo ni milki ya Lebanon

Mara hii pia utawala wa Kizayuni wa Israel kwa himaya ya Marekani unataka kupora eneo kubwa lenye utajiri mkubwa wa gesi na mafuta. Utawala wa Kizayuni unataka kutatua matatizo yake makubwa ya kiuchumi kwa kupora na kukalia kwa mabavu eneo hilo muhimu na lenye utajiri wa nishati katika Bahari ya Mediterania.

Nukta ya tatu ni kuwa, hatua ya Israel kuteka eneo hilo la kijiografia linalozozaniwa ina maana ya kuinyima Lebanon haki ya kuchimba mafuta na gesi katika eneo hilo. Hii ni katika hali ambayo hivi sasa Lebanon inakabiliwa na mgogoro mkubwa kiuchumi na iwapo itaweza kunufaika na mafuta na gesi katika pwani yake ya Bahari ya Mediterania, basi itatatua sehemu kubwa ya matatizo yake ya kiuchumi kama ambavyo Sayyid Hassan Nasrallah alivyosema katika hotuba yake kwamba: "Sisi tuna utajiri mkubwa ambao ndio tumaini pekee la kuiokoa Lebanon kutoka katika migogoro ya sasa ya kiuchumi."

Kwa kuzingatia nukta hiyo, Kiongozi wa Hizbullah amesisitiza umuhimu wa kuuzuia utawala wa Kizayuni wa Israel kuchimba gesi katika eneo linalozozaniwa na kusema kadhia hii ina umuhimu sawa na ile ya kukombolewa mwaka 2000 ukanda wa mpakani uliokuwa unakaliwa kwa mabavu na Israel.

Nukta ya nne katika hotuba ya Sayyid Hassan Nasrallah ni kuwa amefichua njama nyingine ya Marekani dhidi ya Lebanon. Kwa miaka kadhaa sasa Lebanon imekuwa ikikumbwa na mgogoro wa kiuchumi. Marekani imekuwa ikidai kuwa iko tayari kuisaidia Lebanon kukabiliana na matatizo yake ya kiuchumi. Pamoja na hayo ni wazi kuwa Israel inapora utajiri wa Lebanon kwa msaada wa Marekani na hivyo hakuna shaka kuwa Marekani inapanga njama ya kuona Lebanon inakumbwa na njaa na ukata.

Wapiganaji wa Hizbullah

Katibu Mkuu wa Hizbullah amefafanua kuhusu nukta hiyo na kusisitiza ulazima wa kusitishwa uporaji wa utajiri wa Lebanon mara moja kwa kusema: "Kuchelewa hata siku moja kuna maana ya kuangamiza utajiri wa taifa la Lebanon. Israel na Marekani zinalenga kuitumbukiza Lebanon katika njaa na ukata." 

Nukta ya mwisho ni kuwa, ingawa kupora na kukalia kwa mabvu ardhi za wengine ni sifa ya dhati ya utawala wa Israel ambao unapata himaya ya Marekani, lakini katika kadhia ya mzozo huu wa baharini na Lebanon ni wazi kuwa lengo la Marekani na utawala wa Kizayuni ni kuendeleza mgogoro wa kiuchumi katika nchi hiyo sambamba na kuishinikiza harakati ya Hizbullah na pia kuonyesha kuwa harakati hiyo ya mapambano ndiyo inayopaswa kulaumiwa kutokana na hali hii. 

Kwa kuzingatia njama hizo, Sayyid Hassan Nasrallah amesisitiza kwa kusema jukumu kuu la harakati ya Hizbullah ni kusaidia kuihami ardhi, bahari, mafuta, gesi na heshima ya Lebanon. 

 

Tags