Jun 12, 2022 07:53 UTC
  • Wanamuqawama wa Palestina Gaza wafanyia majaribio makombora yao

Duru za kiusalama huko Palestina zimedokeza kuwa, vikosi vya muqawama vya nchi hiyo vimefanyia majaribio makombora yao katika fukwe za Ukanda wa Gaza.

Shirika la habari la Mehr limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, makombora kadhaa yamevurumishwa kwenda baharini kwenye majaribio hayo yaliyofanyika jana Jumamosi.

Maelezo zaidi kuhusu makombora yaliyofanyiwa majaribio na makundi ya muqawama wa Palestina yaliyoshiriki kwenye zoezi hilo la jana hayajatolewa.

Hata hivyo vikosi vya muqawama wa Palestina katika miezi ya hivi karibuni vimefanyia majaribio makombora yao kadhaa, sanjari na kufanya luteka za kijeshi.

Makombora ya wanamuqawama

Duru za habari za lugha ya Kiebrania zimeeleza kuwa, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika miezi ya hivi karibuni limelazimika kusitisha mashambulizi yake dhidi ya mji wa Jenin, likihofia majibu ya makundi ya wanamapambano wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza.

Vikosi vya muqawama vya Palestina vimeonya kuwa, hatua yoyote ya kijeshi ya utawala haramu wa Israel katika mji wa Jenin, haitapita hivi hivi bila kupatiwa jibu kali.

 

 

Tags