Jun 22, 2022 09:45 UTC
  • Malengo tofauti ya safari ya kieneo ya Bin Salman

Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ameanza safari yake ya kieneo kwa kufanya ziara huko Misri na kuzitembelea pia nchi mbili za Jordan na Uturuki.

Safari ya kieneo ya Bin Salman ina malengo tofauti. Lengo la kwanza la ziara hiyo linahusiana na masuala binafsi. Muhammad bin Salman ambaye ni mtu aliye na uchu wa madaraka, kwa karibu miaka minne iliyopita amekuwa chini ya mashinikizo makubwa  ya kisiasa kutoka pande mbalimbali duniani kufuatia tukio la jinai ya kuuliwa kinyama mwandishi habari aliyekuwa akiukosoa pakubwa utawala wa Saudia, Jamal Khashoggi. Bin Salman ambaye alihitajia pakubwa kuonekana katika vyombo vya habari akijipambanua kama kiongozi mpenda mageuzi kwa mara nyingine tena sasa amekuwa akizingatiwa na kupewa uzito mkubwa  na vyombo vya habari; na hivyo kudhihirisha kukubalika kwake pole pole katika nchi za eneo hili kama mfalme ajaye wa Saudi Arabia. Safari ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia imeanza kwa kuitembelea Misri. Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri ndiye aliyemlaki Bin Salman katika uwanja wa ndege wa Cairo. Aidha lengo jingine la Muhammad bin Salman limetajwa kuwa ni kujikurubisha kwa Mfalme wa Jordan na Rais wa Uturuki.  

Muhammad bin Salman akilakiwa Cairo na Rais wa Misri Abdel Fattah al Sisi 

Lengo la pili la Bin Salman katika ziara yake katika eneo limetajwa kuwa ni kwa ajili ya kuimarisha nafasi ya Saudi Arabia katika eneo la Mashariki ya Kati. Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia amefanya ziara huko Misri huku  nchi hiyo ikiwa katika hali ambaya ya kiuchumi.  Licha ya kuwa Misri ilikuwa tayari imeathiriwa na matatizo ya kiuchumi kabla hata ya kuanza vita vya Ukraine, lakini vita hivyo vimeshadidisha matatizo hayo ya kiuchumi. Kuendelea vita vya Russia dhidi ya Ukraine kuimeipelekea serikali ya Misri ishindwe kuendelea kutoa ruzuku kwa baadhi ya bidhaa na huduma kwa jamii. Katika upande mwingine, idara za usalama za nchi hiyo pia zimetahadharisha juu ya uwezekano wa kujiri ghasia na machafuko ya wananchi nchini wanaolalamikia kupanda bei za bidhaa muhimu za mahitajio. 

Cairo inahitajia sana msaada wa fedha ili kukidhi mahitaji yake ya dharura ya kununua haraka chakula khususan baadhi ya bidhaa muhimu kama ngano na nafaka nyingine. Kwa msingi huo, Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri ameziomba nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kubadilisha mitaji yao ya kibiashara  huko Misri na kuwa vitega uchumi. Gazeti la al Arabi al Jadid limeandika katika ripoti yake kwamba: Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) mwezi Mei mwaka huu ziliipatia Misri jumla ya dola bilioni nne kama msaada wa haraka kwa nchi hiyo. Saudia na Imarati zilifanya hivyo zikijibu ombi la Misri la kutaka kupatiwa msaada wa haraka ili kuondakana na hali mbaya ya  kiuchumi inayoikabili. 

Moja ya sababu iliyozipelekea Saudia na Imarati kuisaidia kifedha Misri ni hii kwamba, nchi hizo zina wasiwasi kuwa, Rais Abdel Fattah al Sisi asijeangukia katika hatima sawa na ile iliyompaya dikteta wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak mnamo mwaka 2011. Imaduddin Adeeb mwandishi habari raia wa Misri anayeiunga mkono serikali ya nchi hiyo katika uchambuzi wake chini ya anwani "Ni nani atakayelipa gharama chungu za vita vya Russia na Ukraine kwa Misri?" ameandika: "Iwapo nchi za pambizoni mwa Ghuba ya Uaemi hazitoisadia Misri  uasi na machafuko yataibuka nchini humo sawa na yale yaliyozuka dhidi ya utawala wa Mubarak; matukio ambayo hayatakuwa kwa maslahi ya nchi za Kiarabu za eneo."  

Hosni Mubarak, dikteta aliyeng'olewa madarakani wa Misri 

Kwa msingi huo, kwa upande mmoja Bin Salman amekubali kuisaidia kifedha Misri na wakati huo huo kukiwa pia na uwezekano wa nchi hiyo kuwekeza huko Misri na hivyo Saudia kuweza kuimarisha nafasi yake nchini humo; na katika upande mwingine kwa hatua yake hiyo Saudia itaweza kuzuia kuibuka uasi mpya katika Ulimwengu wa Kiarabu; uasi ambao taathira zake zinaweza kufika pia hadi Saudi Arabia. 

Lengo la tatu la Bin Salman katika ziara yake tajwa ni kuboresha uhusiano kati ya Saudia na Jordan. Jordan tokea mwaka jana wa 2021 imekumbwa na jaribio la mapinduzi yaliyofeli dhidi ya Mfalme Abdallah wa Pili wa nchi hiyo. Baadhi ya duru za habari ziliripoti kuhusu kuhusika Muhammad bin Salman katika jaribio hilo la mapinduzi. Bin Salman anaitembelea Jordan mwaka mmoja baada ya kutekelezwa jaribio hilo la mapinduzi lililogonga mwamba; na hii inaonyesha kuwa Riyadh na Amman ziko katika mkondo wa kuboresha uhusiano kati yazo. Mbali na hilo, Muhammad bin Salman pia mwenyewe anaweza kujivua kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi lililofeli la mwaka uliopita. 

Lengo la nne la safari ya Bin Salman huko Misri, Jordan na Uturuki ni kuratibu misimamo ya nchi za Kiarabu katika kukaribia safari ya Rais Joe Biden wa Marekani. Rais wa Marekani anatazamiwa mwezi ujao wa Julai kufanya ziara huko Riyadh, Saudi Arabia. Inaonekana kuwa matokeo ya ziara ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia huko Misri, Jordan na Uturuki yataathiri maamuzi yatakayochukuliwa katika kikao cha Riyadh kitakachohudhuriwa na Rais Joe Biden kuhusu masuala mbalimbali ya Mashariki ya Kati. Kwa ibara nyingine ni kuwa, Saudi Arabia inahitajia mshikamano na misimamo ya pamoja ya nchi za Kiarabu ili kufikiwa mtazamo wa pamoja kati yazo na Biden; jambo ambalo limezingatiwa katika safari zote za Bin Salman. 

Rais Joe Biden wa Marekani 

Tags