Jun 22, 2022 11:07 UTC
  • Abdul Malik al-Ajri
    Abdul Malik al-Ajri

Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imeikejeli taarifa iliyotolewa na viongozi wa Saudi Arabia na Misri kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni mpango wa Ghuba ya Uajemi kuhusu Yemen.

Ni baada ya safari ya Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman nchini Misri ambako alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo, Abdel Fattah al-Sisi siku ya Jumanne ya jana. Mwishoni mwa mazungumzo hayo pande mbili zilitoa taarifa ya pamoja zikisisitiza udharura wa kuzidisha ushirikiano wa kiuchumi.

Katika sehemu moja ya taarifa hiyo ya Bin Salman na al Sisi inayohusiana na Yemen, pande hizo mbili zimetoa wito wa kuwepo himaya ya kikanda na kimataifa kwa ajili ya kupata suluhisho la kisiasa kwa mujibu wa kile kilichotajwa kuwa ni "mpango wa Ghuba ya Uajemi" na utekelezaji wake. 

Abdul Malik al-Ajri, mjumbe wa timu ya mazungumzo ya Serikali ya Uokoaji ya Kitaifa ya Yemen, amekejeli hatua ya muungano wa vita vya Yemen unaoongozwa Saudia ya kukariri kariri kile kinachoitwa "mpango wa Ghuba ya Uajemi" katika matamshi na taarifa zote, na kuhoji kuwa, je, wanataka kuufanya mpango huo kuwa kipengee cha adhana zinazosomwa misikitini?! Amesisitiza kuwa mpango huo hauna maana.

Bin Salman na al Sisi

Maafisa wa serikali ya Sanaa wamekataa mpango wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi wa kufanyika mazungumzo kati ya pande zinazozozana mjini Riyadh huko Saudi Arabia.

Ni vyema kuashiria kuwa Saudi Arabia iilianzisha vita dhidi ya taifa la Yemen zaidi ya miaka saba iliyopita ikisaidiwa na washirika wake wa kikanda na kimataifa hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.