Jun 23, 2022 12:28 UTC
  • Kiongozi wa HAMAS aonana na Katibu Mkuu wa Hizbullah Beirut

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut.

Kwa mujibu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma ya Hizbullah, katika mazungumzo yake na Ismail Haniya, Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas yaliyofanyika leo mjini Beirut, Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah amesisitiza kustawishwa na kuimarishwa mhimili wa Muqawama,  kufuatiliwa vitisho na changamoto zinazoukabili, kutumiwa fursa zilizopo, kufanyika mazungumzo na kuhusu ulazima wa kuwepo ushirikiano baina ya pande zote za mhimili wa muqawama kwa ajili ya kufanikisha lengo kuu ambalo linahusiana na Quds, matukufu ya Kiislamu na piganio tukufu la Palestina.

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, ambaye amefuatana na ujumbe maalumu wa harakati hiyo katika ziara yake nchini Lebanon, anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo pia na Rais Michel Aoun, Waziri Mkuu Najib Miqati pamoja na Nabih Berri Spika wa bunge la nchi hiyo.

Ziara ya ujumbe wa Hamas nchini Lebanon imefanyika sambamba na kuongezeka mivutano kati ya nchi hiyo na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kufuatia hatua ya Tel Aviv ya kutuma meli yake kwa ajili ya kuchimba gesi katika eneo linalozozaniwa na pande mbili.

Jana Jumatano, Ismail Haniya alikutana na kufanya mazungumzo na Mufti Mkuu wa Lebanon Sheikh Abdulatif Daryan na kumshukuru kwa mchango na misimamo yake ndani na nje ya Lebanon kuhusiana na kadhia ya Quds, suala la Palestina na wananchi wa Palestina.

Katika mazungumzo hayo, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amesisitiza mshikamano na uungaji mkono kamili wa harakati hiyo kwa Lebanon kuhusu haki yake ya kunufaika na maliasili zake ikiwemo ya gesi.../

Tags