Jun 24, 2022 07:11 UTC
  • Nchi za Kiarabu mbioni kuhakikisha Syria inarejeshewa uwanachama wake Arab League

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League amesema nchi kadhaa wanachama wa jumuiya hiyo zinafanya juhudi kuhakikisha Syria inarejeshewa uwanachama wake.

Mnamo mwaka 2011 na kwa mashinikizo ya Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia kufuatia kuanza kwa mgogoro nchini Syria, Arab League ilichukua hatua ya kusimamisha uwanachama wa nchi hiyo ya Kiarabu katika jumuiya hiyo, huku nchi nyingi za Kiarabu zikiamua kufunga balozi zao na kuvunja uhusiano wao wa kidiplomasia na serikali ya Damascus.

Lakini hivi sasa, na baada ya serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria kupata ushindi dhidi ya makundi ya kigaidi na kufeli njama ya pamoja ya Waarabu na Wamagharibi dhidi ya nchi hiyo, jumuiya ya nchi za Kiarabu pamoja na nchi nyingi za Kiarabu zikiwemo za eneo hili zinapigania kuanzisha tena uhusiano na Syria na kufungua tena balozi zao mjini Damascus.

Rais Bashar al Assad wa Syria

Naibu Katibu Mkuu wa Arab League Hossam Zaki amesema, baadhi ya nchi wanachama ikiwemo Algeria zinafanya juhudi kuhakikisha Syria inarejea kwenye jumuiya hiyo na kwamba si baidi tukio hilo likajiri kabla au baada ya kikao kijacho cha wakuu wa Arab League kitakachofanyika mjini Algiers.

Zaki ameendelea kusisitiza kwamba Jumuiya ya Nchi za Kiarabu inakaribisha kurejea Syria katika jumuiya hiyo.

Kitambo nyuma, Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria alieleza kuwa kuziunganisha pamoja tena nchi za Kiarabu kunalazimu kuirejesha Syria katika Aarab League na akasisitiza kwamba hakuna nchi yoyote yenye haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Kikao kijacho cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kimepangwa kufanyika nchi Algeria kuanzia tarehe mosi hadi pili Novemba mwaka huu.../