Jun 25, 2022 03:04 UTC
  • Safari ya Uturuki; Urafiki wa kimbinu kati ya Erdogan na Bin Salman

Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman amefanya safari mjini Ankara na kukaribishwa rasmi na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.

Uhusiano wa Uturuki na Saudi Arabia umeingia katika hatua ya utulivu na suluhu baada ya kipindi cha mvutano na malumbano. Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ambaye hapo awali alikuwa mkosoaji mkuu wa sera ya kigeni ya Saudi Arabia, haswa mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman, mwezi Aprili mwaka huu alilegeza misimamo yake na kwenda Riyadh ambako alikutana na kufanya mazungumzo na Mfalme na Mrithi wa utawala huo. Sasa, Muhammad bin Salman, katika ziara yake mjini Ankara, amejibu ziara ya Erdogan mjini Riyadh kwa lengo la kuboresha na kupanua zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili.

Bila shaka, lengo muhimu zaidi la Bin Salman huko Uturuki ni kutaka kujiondoa hatiani kikamilifu kuhusiana na jinai ya mauaji ya kikatili dhidi ya mwandishi na mkosoaji wa utawala wa Saudia, Jamal Khashoggi. Khashoggi aliuawa na maajenti wa Saudia Oktoba 2018 akiwa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul. Muhammad bin Salman anatumai kuwa, kwa kujiondoa hatiani katika kadhia ya mauaji ya Jamal Khashoggi na kupata uungaji mkono wa Waturuki katika suala hilo, ataweza kujinasua na mashinikizo ya kimataifa yanayomuandama katika  masuala ya haki za binadamu.

Madhumuni mengine muhimu ya safari ya bin Salman nchini Uturuki ni kujitambulisha kama mfalme mtarajiwa wa Saudi Arabia. Kwa maneno mengine ni kuwa, Muhammad bin Salman ambayo anajihisi kuwa ndiye mfalme wa baadaye wa Saudi Arabia, anafanya jitihada za kuboresha nafasi yake ya kikanda na kimataifa kupitia safari hizo hasa kwa kutumia nyenzo za kiuchumi. Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia amefanya safari katika nchi tatu za Misri, Jordan na Uturuki ambazo zote zinasumbuliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi; na Bin Salman anaweza kuimarisha nafasi yake ya kieneo na kimataifa kwa ajili ya kupata kiti cha ufalme wa Saudi Arabia kwa kutoa ahadi za kiuchumi. 

Pamoja na hayo yote inatupasa kusema kuwa safari ya Bin Salman nchini Uturuki imekumbana na ukosoaji mkubwa ndani ya nchi hiyo. Erdogan daima ameonyesha kuwa anabadilisha sera na misimamo yake kulingana na hali ya zama na nafasi yake ya kisiasa. Katika miaka ya hivi karibuni, Erdogan alikuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa sera za Saudi Arabia katika nyanja mbalimbali. Kilele cha ukosoaji huo kilionekana katika kesi ya mauaji ya Jamal Khashoggi. 

Mwaka 2018 Erdogan alisema: "Saudi Arabia imetuomba nyaraka za mauaji ya Khashoggi. Tuko tayari kuwaruhusu kuja hapa na kusikiliza faili za sauti, lakini hatutatoa mafaili hayo kwa Saudi Arabia. Je, wanataka kuua na kuharibu mafaili haya? Ngoja niwaambie. Katika faili hili la sauti, mmoja wa maajenti wa usalama wa Saudia alisema: 'Najua kuikata vipande vipande, sina tatizo!' Hivi mnadhani kuwa sisi ni wajinga tuwatumie mafaili haya?! Waturuki si wapumbavu, na hapana shaka kuwa watawasaili."

Recep Tayyip Erdogan

Hata hivyo, miaka mitatu na nusu baada ya matamshi hayo, Rais huyo huyo wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameamuru jalada lote la kesi hiyo, nyaraka za uchunguzi na ushahidi wa kimahakama wa mauaji hayo vitumwe na kupelekwa Riyadh!

Itakumbukwa kuwa Jamal Khashoggi aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa Muhammad bin Salman na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia aliuawa kinyama ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul na mwili wake ukakatwa vipande vipande. Kubadilika kikamilifu kwa misimamo ya Erdogan kunatokana na matatizo makubwa ya kiuchumi nchini Uturuki yanayosababisha mashinikizo kwa serikali yake. Maono ya Erdogan ni kwamba, anaweza kuboresha nafasi yake katika maandalizi ya uchaguzi wa rais mwakani kwa kurekebisha uhusiano na Saudi Arabia na kuvutia wawekezaji wa kigeni.

Hatua hii ya Erdogan imekabiliwa na ukosoaji mkubwa hususan ndani ya Uturuki kwenyewe. Ahmet Davutoğlu kiongozi wa chama cha Future Party na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Uturuki, alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza waliokosoa vikali sera za Erdogan, akitangaza kwamba kupeleka faili na kesi ya mauaji kwa katili na muuaji mwenyewe ni utovu wa nidhamu ambao utaharibu na kutia doa sura ya Uturuki.

Ahmet Davutoğlu

Kwa kuzingatia haya yote tunaweza kusema kwamba, hatua za Erdogan na Bin Salman na safari za kidiplomasia za pande mbili zinatokana zaidi na "hitaji la kimkakati" la Erdogan na Bin Salman kuliko mabadiliko halisi katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili kuelekea kwenye "urafiki".

Tags