Jun 26, 2022 02:21 UTC
  • Mfalme wa Jordan ataka kuundwa 'NATO ya Asia Magharibi'

Mfalme wa Jordan amesema anaunga mkono wazo la kuundwa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Asia Magharibi, utakaoshabihiana na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO).

Mfalme Abdullah II wa Jordan amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya CNBC News na kueleza kuwa, miungano ya namna hii inaweza kupata mafanikio ikiwa itaundwa na mataifa yenye fikra na mitazamo inayofanana.

Amesema, "ningependa kuona nchi za eneo hili zinaichangamkia kadhia hii. Nitakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kuunga mkono NATO ya Mashariki ya Kati."

Mfalme wa Jordan amesema jambo la kuzingatiwa kabla ya kuundwa muungano huo wa kijeshi ni kuhakikisha kuwa maono na kaulimbiu yake ipo wazi na inafahamika kiwepesi.

Kuparaganyika muungano wa kijeshi wa NATO

Ameashiria operesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine na kubainisha kuwa, vita hivyo tayari vimeyaleta pamoja mataifa ya eneo la Asia Magharibi.

Wazo la kuundwa 'NATO ya Asia Magharibi' na miungano mingine ya kijeshi inayofanana na NATO inayoongozwa na Marekani limeibua tumbojoto miongoni mwa viongozi mbalimbali duniani, ikizingatiwa kuwa mpango wa kutaka kupanua NATO kuelekea upande wa magharibi ya mipaka ya Russia ni moja ya sababu kuu za kuibuka vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine.

Tags