Jun 26, 2022 02:32 UTC
  • Njama mpya za Marekani na Saudi Arabia nchini Syria

Baadhi ya vyanzo vya habari vimeripoti kuwa Marekani na Saudi Arabia zimeanzisha jitihada za pamoja za kuunda upya kikosi kinachojulikana kwa jina la Jaish Maghawir al-Thawra (Jeshi la Makomando wa Mapinduzi) katika kituo cha Al-Tanf kinachosimamiwa na Marekani kilichoko kwenye mpaka wa Jordan, Syrian na Iraq.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, sherehe ya kuhitimu mafunzo wapiganaji wa kikosi hicho zilifanyika hivi karibuni, na baadhi yao wamepelekwa eneo la al Hasakah na waliosalia watajiunga na vikosi vya waasi wa kundi linalojiita Syrian Democratic Forces (SDF) katika maeneo yenye utajiri wa mafuta nchini Syria ili kulizuia jeshi la nchi hiyo kusonga mbele kwa ajili ya kukomboa maeneo hayo. Kamanda wa kikosi hicho pia alitembelea Saudi Arabia wiki mbili zilizopita. Kikosi hicho ambacho kiliundwa na watu waliokimbia jeshi la Syria mwaka 2015, kilikaribia kusambaratika na baadhi ya wapiganaji wake waliamua kujisalimisha kwa jeshi la taifa kwa kuhofia hatima mbaya. Kwa msingi huo hata kama kikosi hicho kitahuishwa tena hakitaweza kuleta mabadiliko yoyote katika mlingano wa kijeshi nchini Syria. Hata hivyo juhudi za Marekani na Saudi Arabia za kutaka kuunda tena kikosi hicho zina ujumbe na nukta muhimu unaofungamana na mlolongo wa mabadiliko makubwa yanayojiri katika eneo la Magharibi mwa Asia na ulimwenguni kwa ujumla.

Miongoni mwa nukta hizo ni kwamba, baada ya kuanza vita vya Ukraine kumekuwepo wasiwasi kwamba yumkini taathira zake mbaya zikaathiri pia hali ya Syria. Kwa kuzingatia haja ya nchi za Magharibi na NATO kwa Uturuki katika mgogoro wa Ukraine, Ankara inalitumia suala hilo kama wenzo wa mashinikizo wa kupanua satua na ushawishi wake huko Syria na vilevile udhibiti wake katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na waasi wa Kikurdi wanaosaidiwa na Marekani. Katika mkondo huo baadhi ya ripoti zinasema, katika siku za karibuni Uturuki imekuwa ikifanya jitihada za kuanzisha ukanda wa amani huko Syria. Hivyo Marekani ambayo inaihitajia sana Uturuki katika kipindi cha sasa na inafanya mikakati ya kufanya suluhu baina ya nchi hiyo, utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia, haitaki kukabiliana na Uturuki huko Syria; na sasa imeamua kuwaweka vibaraka wake wapya wa Jaish Maghawir al-Thawra (Jeshi la Makomando wa Mapinduzi) badala ya waasi wa Kikkurdi wa Syrian Democratic Forces (SDF) katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Syria ili kuiridhisha Uturuki.

Katika upande mwingine, tangu kuanza kwa vita vya Ukraine, Wamagharibi wamekuwa wakifanya juhudi za kuitumi Syria kama uwanja wa kulipiza kisasi dhidi ya Russia kutokana na kushindwa kwao huko Ukraine. Japokuwa Saudi Arabia awali ilijidhihirisha kuwa haipendelei upande wowote katika vita vya Ukraine, lakini ishara na harakati zote ikiwa ni pamoja ya safari ya karibuni ya Joe Biden nchini Saudi Arabia na hatua ya Riyadh ya kuzidisha uzalisha wa mafuta ili kufidia upungufu wa nishati katika masoko ya Ulaya uliosababishwa na vita vya Ukraine na kushirikiana na Marekani katika kuunda tena kikosi cha waasi huko Syria, yote haya yanaonesha kwamba, utawala huo wa kifalme umerejea tena katika mzingo wa Marekani.

Bin Salman na Biden

Kuna masuala kadhaa ambayo yanayoweza kuashiriwa kuhusiana na misimamo ya sasa ya Saudia. Kwanza ni kwamba, Syria- tofauti na matakwa ya Riyadh- imekataa kubadilisha msimamo wake wa kuendelea kushikamana na kambi ya Muqawama na imekataa kubadili msimamo huo licha ya mashinikkizo, vita na hasara kubwa ya hali ya mali. Pili ni kwamba, baada ya makubaliano ya kusitisha vita huko Yemen, Saudia inajihisi kupungukiwa na mashinikizo na mzigo wa vita. Na tatu ni kwamba, kutokana na kuongezeka bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa na kuzidishwa kiwango cha mauzo ya bidhaa hiyo, Saudia imeingiza pato zaidi la fedha za kigeni. Hata hivyo badala ya kujifunza na kupata ibra kutokana na yaliyowakuta katika miaka iliyopita, watawala wa Riyadh wameamua tena kutekeleza siasa za kuingia masuala ya ndani ya nchi nyingine wakifuata kibubusa sera na maamuzi ya mabwana zao na kujikurubisha zaidi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa kutilia maanani hayo yote, tunaweza kusema kuwa, juhudi za Marekani na Saudi Arabia za kuunda upya kikosi cha wapiganaji vibara na waasi huko Syria ni kieleleo cha faili na mpango mpya unaosukwa na mabeberu na vibaraka wao wa kikanda.  

Tags