Jun 26, 2022 07:44 UTC
  • Sanaa yalalamikia vikwazo vya Riyadh dhidi ya mahujaji wa Yemen

Afisa wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amepinga masharti na vikwazo ambavyo Saudi Arabia imewawekea mahujaji wa Yemen.

Ripoti zinasema kuwa, askari usalama wa Saudia wamekamata mahujaji kadhaa kutoka nchi kama vile Misri, Libya, Yemen na Syria katika ibada ya Hija ya mwaka huu huko katika ardhi tukufu ya Makka.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Abdul Rahman Al-Nami, Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Hija na Umrah katika Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen, amesema utawala wa Saudi Arabia umeruhusu mahujaji 11,000 pekee wa Yemen kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu.

Al-Nami ameongeza kuwa, Saudi Arabia pia imewekea masharti na vikwazo vingi mahujajii wa Yemen, vikiwa ni pamoja na kuwa na umri wa chini ya miaka 65, kuwa na hati ya kusafiria iliyotolewa  Aden (makao makuu ya serikali iliyojiuzulu ya Yemen inayoongozwa na Riyadh) na ongezeko la asilimia 100 la gharama ya Hija. 

Hivi majuzi, taasisi za kutetea haki za binadamu na za kisiasa, wasomi, wahubiri na shakhsia wengi wa Ulimwengu wa Kiislamu walianzisha kampeni dhidi ya hatua ya utawala wa Saudi Arabia ya kuhusisha ibada ya Hija na na Umra na masuala ya "kiusalama".