Jun 27, 2022 01:22 UTC
  • Kuimarishwa ushirikiano wa kiusalama na kiintelijensia kati ya Uturuki na utawala bandia wa Israel

Katika hali ambayo utawala wa Kizayuni wa Israel umesisitiza kuwa hauko tayari kuipatia fursa za upendeleo Uturuki hususan katika usafirishaji gesi kwa ajili ya nchi za Umoja wa Ulaya ili kustawishwa uhusiano baina yao, serikali ya Recep Tayyip Erdoğan ingali inaendelea kupaparika upande wake kutaka kupanua na kustawisha uhusiano na utawala huo wa ubaguzi wa rangi.

Katika kutilia mkazo mtazamo huo wa serikali ya Ankara, wakati waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alipofanya mkutano na waandishi wa habari mjini humo hivi karibuni akiwa na mwenzake wa utawala wa Kizayuni Yair Lapid alitangaza kuwa, hatua za Uturuki za kuongeza kiwango cha uwakilishi wa kidiplomasia na Tel Aviv zimeanza katika ngazi ya ubalozi.

Halikadhalika, waziri huyo wa mambo ya nje wa Uturuki alisisitiza kwa kusema:

Uturuki haitaruhusu kufanyika mashambulio ya kigaidi katika ardhi yake na iko tayari kuimarisha zaidi mashirikiano ya kiusalama na kiintelijensia na Israel.

Cavusoglu (kushoto) na Lapid walipokutana Tel Aviv kabla ya Ankara

Kabla ya kauli yake hiyo Mevlut Cavusoglu alikuwa ameshatoa mwito pia wa kustawishwa mashirikiano na utawala wa Kizayuni katika nyanja za nishati, biashara, uwekezaji, sayansi na teknolojia, kilimo na usalama wa chakula.

Juhudi za serikali ya Uturuki za kupanua na kustawisha uhusiano na Israel zinaendelezwa ilhali  maafisa wa serikali ya Erdoğan wamekuwa wakidai kila mara kwamba, serikali hiyo ni mtetezi wa taifa linalodhulumiwa la Palestina. Lakini baada ya kufungwa ofisi za uwakilishi za Harakati ya Palestina ya Hamas na kufukuzwa wawakilishi wa serikali na wananchi wa Palestina nchini Uturuki, imedhihirika kuwa sera za serikali ya Ankara hubadilika kulingana na maslahi ya chama tawala cha nchi hiyo. Sambamba na hilo, imebainika pia kwamba kupigia upatu kadhia ya kuwaunga mkono watu wa Palestina ni mchezo tu unaochezwa na viongozi wa Uturuki kwa lengo la kujitangaza katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na mbele ya macho ya mataifa ya Waislamu. Lakini hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na viongozi wa chama tawala cha Uadilifu na Ustawi cha Uturuki zimethibitisha ukweli kwamba, kitu pekee wanaochofikiria wanasiasa wanaotawala Uturuki ni namna ya kufanikisha maslahi ya kichama na kujipatia umaarufu miongoni mwa matabaka ya Waturuki walioshika dini. Ni kwa sababu ya kufuatwa sera hizo zisizo za kudumu na za kujali maslahi tu na wanasiasa Waislamu hasa wa Uturuki ndio maana utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ungali unaendeleza bila hofu wala kiwewe mauaji ya wananchi madhulumu na wasio na ulinzi wa Palestina. Ahad Mohammadli, amekosoa  kimya cha baadhi ya serikali za nchi za Kiislamu kuhusiana na jinai zinazofanywa na wazayuni katika Quds tukufu, hususan kimya cha Uturuki na Jamhuri ya Azerbaijan kwa kusema:

"Katika miaka iliyopita, kimya cha serikali zinazojidai kuwa na Uislamu, kimepelekea kushtadi jinai za Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina".

Erdogan (kulia) na Herzog mjini Ankara

Hatuwezi kuukana ukweli kwamba, baada ya viongozi wa Ankara kugonga mwamba katika kutatua migogoro ya mtawalia ya kiuchumi ya ndani ya Uturuki wameamua kuanzisha ushirikiano na utawala wa Kizayuni. Kwa hakika moja ya malengo ya viongozi wa Uturuki ya kupanua uhusiano na Israel ni kutatua matatizo ya kiuchumi na kuipatia suluhisho hali mbaya ya kifedha pamoja na matatizo mengine ambayo yameathiri mno hali ya maisha ya raia wa nchi hiyo. Lakini pamoja na hayo, misimamo iliyochukuliwa hivi karibuni na viongozi wa Israel inaonyesha kwamba, utawala huo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid hauko tayari kuipatia Uturuki fursa yoyote ya upendeleo kwa ajili ya kutatua matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo. 

Mfano mmoja tu wa msimamo huo ni kufanyika mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Israel na Cyprus. Kwa hakika kufanyika manuva hayo baina ya utawala wa Kizayuni na Cyprus ya Kusini iliyopo upande wa Ugiriki kumewatia wasiwasi viongozi wa Uturuki. Mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi yaliyofanyika mwezi uliopita wa Mei na kuchukua muda wa siku tano hayakuwafurahisha viongozi wa serikali ya Ankara, kiasi kwamba katika hatua ya kwanza ya kuonyesha msimamo, tena laini, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uturuki Tanju Bilgic alisema:

Tanju Bilgic

"Kwa mara nyingine tena tunawataka watu wanaoshiriki katika hatua kama hizi za serikali ya Cyprus ya Kusini, wasikubali kutumiwa na kuwa wenzo wa hatua hizi za kichochezi na kipropaganda".

Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, uhusiano wa Uturuki na Israel umeshuhudia shwari na dhoruba nyingi. Sababu kuu ya kuwepo kwa hali hiyo ni maonyesho ya maafisa wa serikali ya Erdoğan ya kujifanya watu wenye misimamo huru katika maamuzi yao. Wakati utawala haramu wa Israel ulipoishambulia meli ya Uturuki ya Mavi Marmara iliyokuwa imekusudia kupeleka misaada kwa Wapalestina waliowekewa mzingiro katika Ukanda wa Gaza, maafisa wa serikali ya Erdoğan walijitahidi sana kuhakikisha kadhia hiyo inafikishwa mbele ya jamii ya kimataifa na Baraza la Usalaama la Umoja wa Mataifa. Na kuna wakati viongozi wa Ankara waliliibua katika vyombo vya habari suala la kulipwa fidia na Israel kutokana na hujuma hiyo kwa namna ya kutaka ionekane kwamba, utawala huo wa Kizayuni ndio ulioshindwa katika kadhia hiyo. Lakini si tu Uturuki haikulipwa fidia yoyote, bali utawala dhalimu wa Israel ulitumia kisingizio cha kulinda usalama wake kama hoja ya kuhalalisha mauaji ya raia tisa wa Uturuki na kuihitimisha kadhia hiyo kwa manufaa yake.

Waturuki tisa waliouliwa shahidi na askari wa Kizayuni katika hujuma dhidi ya meli ya Mavi Marmara

Katika hali na mazingira hayo, viongozi wa serikali ya Erdoğan walijaribu kuonyesha kwamba uhusiano baina ya pande mbili umeshavunjwa kikamilifu. Lakini licha ya madai hayo, hivi sasa vyombo vya habari vya Ankara na Tel Aviv vinaripoti kuwa, kwa muda wote wa muongo mmoja uliopita yamekuwepo mashirikiano mapana ya kiusalama na kiintelijensia kati ya pande mbili.

Kwa hakika tunaweza kuthubutu kusema kwamba, katika muda wote huo uhusiano wa Uturuki na Israel haukuvunjwa, isipokuwa ulipunguzwa hadi kiwango cha chini kabisa katika upeo wa vyombo vya habari.../