Jun 27, 2022 03:52 UTC
  • Hania: Makombora 150 yatausambaratisha utawala wa Kizayuni chini ya dakika tano

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ameeleza kuwa, msikiti wa al Aqsa unakaribia kukombolewa na kusisitiza kuwa, makombora 150 yatauangamiza utawala wa Kizayuni katika muda wa chini ya dakika tano.

Msikiti Mtakatifu wa al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu umegeuzwa kuwa eneo la wanajeshi na walowezi wa Kizayuni kwa ajili ya kupoteza utambulisho wa Kiislamu na wa Kikristo wa Baitul Muqaddas na badala yake kuubadili msikiti huo kwa kupachika nembo za Kizayuni. Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) mwezi Oktoba mwaka 2017 lilitangaza kuwa msikiti wa al Aqsa ni mali ya Waislamu na hauna uhusiano wowote na Wayahudi. 

Msikiti wa al Aqsa huko Palestina 

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, Ismail Hania Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ameashiria katika Mkutano wa Kitaifa wa Kiislamu uliofanyika Jumamosi huko Beirut mji mkuu wa Lebanon chini ya anwani: "Hiyo Tunaiona Kwa Karibu", namna upanga wa Quds utaendelea kufanya kazi hadi kukombolewa kikamilifu Palestina na kueleza kuwa: Mji wa Quds na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika miaka iliyopita imekuwa chini ya mashinikizo ili kuwafanya Wapalestina waachane na harakati zao za muqawana na kukimbia ardhi zao.  

Hania ameongeza kuwa, msikiti wa al Aqsa kamwe si wa Wazayuni wala Wayahudi na kusisitiza kuwa, muqawama utasambaratisha matarajio ya Wazayuni. Wakati huo huo amesema, yuko pamoja kikamilifu na Lebanon mkabala wa mashambulizi na chokochoko za utawala wa Kizayuni dhidi ya maliasili za  nchi hiyo na kubainisha kuwa utawala wa Kizayuni hauna haki yoyote katika maji ya Lebanon kama ambavyo haina haki pia huko Palestina.