Jun 28, 2022 09:56 UTC
  • Hamas: Jamii ya kimataifa ikomeshe uchokozi wa Wazayuni

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeitaka jamii ya kimataifa itekeleze wajibu wake wa kusimamisha hujuma ya Wazayuni katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds (Jerusalem).

Taarifa ya harakati ya Hamas iliyotolewa leo kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 55 tangu utawala wa Kizayuni wa Israel ulipolwaa na kughusubu eneo la Quds Mashariki, imetaka kukomeshwa uvamizi wa utawala huo katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.

Tarehe 27 Juni 1967, Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel liliafiki mpango wa kuunganishwa eneo la Quds Mashariki (Jerusalem) na utawala huo, na kwa msingi huo eneo hilo linakaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Hamas imesisitiza kuwa, Quds ni sehemu muhimu ya ardhi ya kihistoria ya Palestina, na Msikiti wa Al-Aqsa ndiyo moyo wake, na kwamba utawala huo ghasibu hauna mamlaka katika eneo hilo, na juhudi zake za kuangamiza utambulisho wa Kiarabu na Kiislamu wa Quds hazitafanikiwa kamwe, na kwamba Quds itabaki kuwa mji mkuu wa milele wa Palestina.

al Aqsa

Hamas imeutaka Umma wa Kiarabu na Kiislamu kufanya harakati za kisiasa, kidiplomasia, za vyombo vya habari na za kibinadamu ili kuimarisha mapambano ya wananchi wa Palestina ya kurejesha haki na kukomboa ardhi na matukufu ya taifa hilo.

Mji wa Al-Quds ulio na Msikiti wa Al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu, ni sehemu muhimu ya Palestina na moja ya maeneo matakatifu ya Kiislamu.

Kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu jinai za Israel, ikiwemo kuwatimua Wapalestina katika ardhi na makazi yao, kinautia utawala huo kiburi zaidi cha kuendeleza uhalifu na jinai hizo.