Jun 29, 2022 10:49 UTC
  • Zaidi ya Wayemeni milioni 19 wanakabiliwa na njaa huku misaada ikipunuga

Wakati Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) likitangaza upunguzaji mkubwa wa msaada wa chakula nchini Yemen, ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inasema zaidi ya Wayemeni milioni 19 sasa wanakabiliwa na njaa, na hivyo kuweka rekodi mpya tangu kuanza kwa vita vikali vinavyoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen ambavyo vilianza mwaka 2015.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema Jumanne kwamba kupunguzwa kwa ufadhili kunatatiza uwezo wake wa kusaidia watu wanaohitaji msaada.

"Watu milioni tano sasa watapokea chini ya nusu ya mahitaji yao ya kila siku, na watu milioni 8 watapata chini ya theluthi moja ya mahitaji yao ya kila siku," OCHA imesema.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu imeeleza kuwa mwezi wa Disemba mwaka jana, Mpango wa Chakula Duniani ulilazimika kupunguza mgao wa chakula kwa watu milioni 8 kutokana na mapungufu ya ufadhili na ilibidi kuanzisha awamu nyingine ya kupunguza chakula mwezi uliopita.

WFP ilitangaza Jumapili kwamba ililazimika kupunguza zaidi misaada ya chakula nchini Yemen kutokana na kutopokea fedha za kutosha, hali ya uchumi wa dunia, na kuendelea kwa athari za vita vya Ukraine.

Mtoto mwenye utapiamlo shadidi Yemen

"Mapungufu makubwa ya ufadhili, mfumuko wa bei duniani na athari za vita vya Ukraine vamelazimisha WFP nchini Yemen kufanya maamuzi magumu sana kuhusu msaada tunaotoa kwa walengwa wetu," shirika hilo lilisema kwenye Twitter.

OCHA pia imesema UNICEF huenda ikalazimika kusitisha matibabu kwa zaidi ya watoto 50,000 walio na utapiamlo uliokithiri ifikapo Julai, na kuongeza kuwa shirika la Umoja wa Mataifa litasitisha msaada wa afya ya uzazi na mtoto ambao utawasaidia hadi watoto milioni 2.5 na wanawake 100,000 kufikia wakati huo.

Umoja wa Mataifa umeielezea hali ya Yemen kuwa "mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani," uliosababishwa na miaka saba ya vita na mzingiro mkali ulioanzishwa na Saudia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo maskini ya Asia Magharibi.

Tangu wakati huo muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umezuia mara kwa mara misaada ya kibinadamu inayohitajika na mafuta kwenye bandari za Yemen.