Jun 30, 2022 02:16 UTC
  • Changamoto kuu zinazomkabili Najib Miqati katika kuunda serikali mpya ya Lebanon

Tangu siku ya Alkhamisi ya tarehe 23 Juni, Rais Michel Aoun wa Lebanon alimkabidhi Najib Miqati, mfanyabiashara mkubwa anayetokea mji wa Tripoli na mwenye umri wa miaka 66, jukumu la kuunda serikali mpya ya nchi hiyo.

Miqati amekuwa waziri mkuu wa muda wa Lebanon kuanzia Septemba 2021 hadi sasa. Jukumu muhimu zaidi alilotekeleza waziri mkuu huyo wa muda katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita lilikuwa ni kuendesha zoezi la uchaguzi wa bunge ambao ulifanyika tarehe 15 Mei mwaka huu. Hivi sasa Najib Miqati ametangazwa kuwa waziri mkuu wa kudumu atakayeshika wadhifa huo kwa muda wa miaka minne. Katika muhula wake huu mpya ya uongozi, Miqati anakabiliwa na changamoto kubwa kadhaa, zikiwemo za uga wa uchumi na ambazo zimekuwepo pia tokea huko nyuma.

Bunge la Lebanon lina wabunge 128. Kwa kura 58 za waliomuunga mkono, Miqati alimshinda mpinzani wake Saleh Nawaf Salam, balozi wa zamani wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa ambaye alipata kura 25. Wabunge wengine 46 waliamua kutopiga kura katika zoezi la kumchagua waziri mkuu mpya. Kura alizopata Najib Miqati zinaonyesha kuwa, waziri mkuu huyo mpya wa Lebanon haungwi mkono na Saudi Arabia na waitifaki wake wa Kiarabu, kwa sababu mshindani wake ndiye aliyekuwa akiungwa mkono na Riyadh. Kwa upande mwingine, matokeo ya uchaguzi wa waziri mkuu yanadhihirisha kwamba, kura ya kuwa na imani na Miqati inalegalega kwa sababu kati ya wabunge wote 128, wabunge 74 hawakumpigia kura za kuwa na imani naye.

Jambo hili linabainisha nukta nyingine muhimu, nayo ni kwamba Najib Miqati atakuwa na kibarua kigumu cha kuunda serikali mpya, kwa sababu wabunge wasiopungua 74 kutoka mirengo tofauti ya Lebanon hawaungi mkono uwaziri mkuu wake. Kwa kuzingatia kwamba ugawaji wa nyadhifa za kisiasa ndani ya Lebanon unafanywa kimafungu, Miqati atalazimika kutafuta ridhaa ya karibu mirengo yote ya kisiasa kwa ajili ya kuunda serikali mpya, jambo ambalo litaufanya uundaji wa serikali hiyo uwe mgumu. Kwa sababu hiyo, Wael Najm, mchambuzi wa masuala ya kisiasa ya Lebanon anaitakidi kuwa, kutokana na mgao wa viti ulivyo ndani ya bunge la Lebanon na tofauti za mitazamo zilizopo kati ya mirengo mbalimbali uundaji wa baraza jipya la mawaziri utakabiliwa na vizuizi vikubwa.

Kuna baadhi ya wachambuzi ambao wanatabiri kuwa, kwa vile uundaji wa serikali mpya ni mgumu na unaweza ukachukua muda mrefu, kuna uwezekano Miqati akalazimika kulifanyia mabadiliko tu baraza lake la sasa la mawaziri na kuliwasilisha bungeni ili kupigiwa kura. Amin Qamuriyah, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, yeye ametabiri kuwa, Najib Miqati hatafanikiwa kuunda serikali kutokana na muda alionao; na badala yake huenda akalazimika kulifanyia mabadiliko baraza lake la sasa la mawaziri, jambo ambalo bila shaka litahitaji ridhaa ya bunge. Hatua hiyo pia haitakuwa sawa na kupigiwa kura ya kuwa na imani na bunge, kwa sababu serikali ya sasa ya Miqati ilishapigiwa kura ya kuwa na imani nayo na bunge lililopita.

Bunge la Lebanon

Changamoto nyingine muhimu itakayomkabili Najib Miqati ni kumalizika muhula wa urais wa Michel Aoun. Kwa mujibu wa katiba, muhula wa urais wa Lebanon ni miaka sita; na kipindi cha urais wa Aoun kinamalizika Oktoba 31 mwaka huu. Michel Aoun alichaguliwa kuwa rais wa Lebanon mwaka 2016 na baada ya mgogoro wa kisiasa wa kumchagua rais uliodumu kwa miezi 29. Kwa kuzingatia mgawanyiko wa kura za mirengo ya Kikristo katika bunge la Lebanon, inavyoonekana mchakato wa kumpata rais mpya ambaye inapasa awe Mkristo utageuka tena kuwa changamoto ya kisiasa katika nchi hiyo; na jambo hilo pia linaweza kuathiri utendaji wa serikali ya Miqati.

Michel Aoun

Mbali na changamoto zote hizo tulizoashiria, "changamoto mama" inayoikabili serikali ya Najib Miqati ni mgogoro wa kiuchumi ulioigubika Lebanon hivi sasa. Kwa zaidi ya miaka miwili na nusu, nchi hiyo inasokotwa na hali mbaya sana ya kiuchumi, kuporomoka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo kulinganisha na dola ya Marekani, uhaba wa fueli na dawa na ongezeko la bei za bidhaa za vyakula. Benki ya Dunia imeutaja mgogoro wa sasa wa kiuchumi wa Lebanon kuwa ni hali mbaya zaidi ya kicuhumi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika karne moja iliyopita. Endapo hautapatikana mwafaka wa kisiasa wa kuunda serikali mpya ya Miqati na vilevile katika kumpitisha rais mpya wa Lebanon, mawili hayo yanaweza kuufanya mgogoro wa sasa wa kiuchumi ufikie kwenye hali tata na mbaya zaidi.../    

Tags