Jun 30, 2022 08:09 UTC
  • Ansarullah: Uwezo wa jeshi la Yemen umepiku wa nchi nyingi za Kiarabu

Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amepongeza hatua kubwa iliyopigwa na nchi hiyo katika kujizalishia makombora ya balestiki ya masafa marefu na kusisitiza kuwa, uwezo wa jeshi la Yemen unazipiku nchi nyingi za Kiarabu.

Abdulmalik Badruddin al Houthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen alisema hayo jana katika hotuba iliyorushwa hewani mubashara kutoka Sanaa, mji mkuu wa Yemen, akiongea na kundi la viongozi wa kikabila kutoka mkoa wa kaskazini wa Hajjah.

Ameeleza bayana kuwa, "Hivi sasa tunazalisha makombora ya balestiki ya masafa marefu ambayo yanaweza kupiga ndani kabisa katika nchi wanachama wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia Arabia."

Amesema uzalishaji wa aina mbalimbali za makombora unaendelea, na sekta hiyo inaendelea kuimarika siku baada ya siku. Amefafanua kwa kusema: Makombora ya Yemen yanazidi kuimarika, kuboreka na kuwa na uwezo wa kulenga shabaha kwa ustadi zaidi.

Abdulmalik Badruddin al Houthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen

Al-Houthi amesema wananchi wa Yemen wataendelea na njia yao ya muqawama kwa ajili ya kufikia mamlaka ya kujitawala, uhuru na kuzuia kikamilifu uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yao.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameeleza kuwa, taifa la Yemen licha ya changamoto zinazolikabili, lakini limepigia hatua kubwa katika uga wa kijeshi, na kwamba hivi sasa linajizalishia silaha anuwai kuanzia bastola, bunduki za Kalashnikov, makombora, vifaru, na zana nyingine mbalimbali za kijeshi.