Jun 30, 2022 13:32 UTC
  • Hamas yawataka Wapalestina kudumisha mapambano ya silaha dhidi ya Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) yenye makao yake katika mji wa Gaza imewahimiza Wapalestina kuendeleza mapambano ya silaha dhidi ya uvamizi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, baada ya mmoja wa makamanda wa jeshi la utawala huo ghasibu kujeruhiwa kwa risasi katika mapigano huko Nablus.

Katika taarifa yake ya leo Alhamisi, msemaji wa Hamas, Fawzi Barhoum amepongeza mapambano ya Wapalestina huko Nablus na kusema "makabiliano endelevu, ya pande zote na yasiyo na kikomo dhidi ya utawala ghasibu wa Israel yanapaswa kuendelezwa na kuzidishwa katika miji na vijiji vyote vya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan."

Barhoum aliendelea kubainisha kuwa, lengo la mapambano hayo ya silaha ni kuzima njama za utawala huo ghasibu, kuudhoofisha na kuzuia kufikiwa kwa malengo yake, hadi ardhi ya Palestina itakapokombolewa kikamilifu.

Jana usiku (Jumatano usiku) mamia ya Wazayuni walivamia kaburi la Nabii Yusuf huko Nablus, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ambapo walikabiliwa na wanamapambano wa Palestina waliowafyatulia risasi na kujeruhi wavamizi watatu akiwemo kamanda wa kikosi cha jeshi la Israel, Roy Zweig.

Hamas yawahimiza Wapalestina kudumisha mapambano ya silaha dhidi ya Israel

Eneo hilo la Joseph’s Tomb linadhibitiwa na Mamlaka ya Palestina; hata hivyo, jeshi la Israel linawaruhusu walowezi kuvamia eneo hilo bila kibali, na hata kuwasindikiza hadi mahali hapo.

Msemaji wa Hamas amesema kuwa: "Kukiri kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba kamanda wake amejeruhiwa katika makabiliano hayo kunaonyesha kuwa muqawama wa Palestina una nguvu za kutosha kuweza kusababisha hasara kwa adui, kuulazimisha utawala huo kanuni mpya za mapambano na kuzidisha gharama za uvamizi wowote wa Israel unaolenga taifa la Palestina."