Jul 02, 2022 11:48 UTC
  • Ukatili ambao Wazayuni wanawafanyia Wapalestina ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa

Mwakilishi wa kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema, ukatili wa mtawalia na wa kimfumo ambao utawala haramu wa Kizayuni wa Israel unawafanyia Wapalestina ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Katika kuhakikisha unafikia malengo yake ya kujipanua, utawala wa Kizayuni kila siku unavamia maeneo tofauti ya Palestina na kuwaua shahidi, kuwajeruhi au kuwatia nguvuni Wapalestina.

Tangu ulipoanza mwaka huu wa 2022 hadi sasa, Wapalestina zaidi ya 60 akiwemo mwandishi wa habari wa televisheni ya Aljazeera Shireen Abu Akleh wameuliwa shahidi na Wazayuni.

Katika ujumbe aliomtumia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na marais wa Baraza la Usalama na Baraza Kuu la umoja huo, Riyadh al Mansour ameeleza kwamba, ukatili wa mtawalia na wa kimfumo ambao utawala haramu wa Kizayuni wa Israel unawafanyia Wapalestina ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa likiwemo azimio 2234 la Baraza la Usalama ambalo limetaka zichukuliwe hatua za haraka za kuzuia aina zote za utumiaji mabavu na kufanya ukatili dhidi ya raia.

Riyadh al Mansour

Al Mansour amesisitiza pia kuhusu ulazima wa jamii ya kimataifa na hasa Baraza la Usalama kuchukua hatua za maana na za uwajibikaji za kutekeleza sheria za kimataifa ambazo zinakiukwa vikali na Israel na akaongezea kwa kusema, ni kwa kuchukuliwa hatua hizo ndipo itawezekana kulinda maisha ya raia wasio na hatia na vilevile kuhitimisha ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Israel ikiwemo mzingiro usio wa kibinadamu dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Tangu mwaka 2006 na baada ya Harakati ya Hamas kushinda uchaguzi wa bunge la Palestina, utawala dhalimu wa Israel umeliwekea mzingiro eneo la Ukanda wa Gaza na unazuia bidhaa muhimu zikiwemo za fueli, chakula, dawa na vifaa vya ujenzi kuingizwa katika eneo hilo.../