Jul 03, 2022 02:13 UTC
  • Wanawake wa Afghanistan wakosoa kutoalikwa katika kikao cha Loya Jirga

Wanawake wa Afghanistan wamekosoa kufanyika kikao cha maulamaa wa kidini wa Baraza la Ushauri kwa ajili ya amani ya Afghanistan (Loya Jiirga) bila ya wanawake wa nchi hiyo kuhudhuria. Kutoshirki wanawake katika kikao hicho kunamaanisha kupuuzwa nusu ya jamii ya watu wa Afghanistan.

Kikao cha siku tatu cha faragha cha Loya Jirga kimefanyika  Kabul mji mkuu wa Afghanistan tangu juzi Alhamisi kwa kuhudhuriwa na shakhsiya na maulamaa mbalimbali wa kidini wa nchi hiyo. Mula Hibatullah Akhundzada  Rais wa kundi la Taliban linaloongoza nchini humo pia anashiriki katika kikao hicho cha siku tatu. 

Mula Hibatullah Akhundzada, Rais wa Taliban  

Hamid Karzai, rais wa zamani wa Afghanistan ndiye aliyetoa pendekezo kwa kundi la wanamgambo wa Taliban kuhusu kuendesha vikao mbalimbali vya viongozi wa makabila chini ya anwani "Loya Jirga" ili waweze kupata uhalali na itibari ndani ya nchi kwa kuitishwa vikao hivyo; jambo ambalo lina tajiriba ya kihistoria huko Afghanistan. Hata hivyo kundi la Taliban limewabadilisha wajumbe wa baraza hilo la jadi na kuwaalika maulamaa katika ukumbi wa Loya Jirga, huku likitafuta tu uhalali wa kidini na kupata baia kutoka kwa wanazuoni na maulamaa wa Kiafghani kote nchini ili kuweza kukubalika nchini. 

Pamoja na hayo, hakuna taarifa zozote kuhusiana na mitazamo ya maulamaa wa kidini wa Taliban katika kikao hicho kuhusu uongozi wa Taliban huko Afghanistan. Aidha kile ambacho kimeripotiwa na taasisi zenye mfungano na Taliban ni uungaji mkono wa makundi yenye misimamo mikali kwa utawala wa kundi hilo na hotuba ya Rais wa Taliban ambayo hata hivyo haikuashiria chochote kuhusu kurejeshwa demokrasia huko Afghanistan. Ahmad Saidi mchambuzi wa masuala ya kisiasa raia wa Afghanistan anasema kuhusu suala hilo kwamba: Taliban inafanya kila iwezalo ili kupata uhalali na kuungwa mkono ndani ya nchi kwa kuitisha kikao hicho tajwa cha maulamaa wa kidini na kuwataka walibai kundi hilo." Hilo si baraza la Loya Jirga linalokusudiwa na wanasiasa ili kufanikisha uundaji wa serikali jumuishi huko Afghanistan."  

Hata kama kwa mtazamo wa fiqhi ya Kitaliban katika jamii ya Afghanistan wanawake wana majukumu na kazi nyingine ghairi ya masuala ya kisiasa na kiidara lakini sambamba na masuala hayo ya kisheria kile kilicho na umuhimu kwa ajili ya wananchi wa Afghanistan ni kuheshimiwa haki za msingi za kila raia wa nchi hiyo katika ngazi zote za kijamii, kisiasa na kiidara. Suala hili lina umuhimu kwa sababu wanawake wa Kiafghani katika miaka ya karibuni wamepiga hatua na kustawi katika sekta mbalimbali za kisayansi, kijamii, kitamaduni na hata za uwakilishi bungeni na kisiasa. Mbali na hayo, kundi la Taliban ambalo limeshika hatamu za uongozi huko Afghanistan linahitaji kuzingatia vigezo na misingi ya utawala inayokubaliwa kimataifa na nchi za Kiislamu; muhimu kuliko yote ikiwa ni kuheshimu haki za raia wote wakiwemo wanawake ili kujinasua katika hali ya kutengwa.  Hii ni kwa sababu nusu ya muundo wa jamii ya Afghanistan inatokana na wanawake; ambapo ipo haja ya kutambua na kuzingatia haki zao za msingi katika nyuga zote ikiwemo katika suala la kuwapatia elimu na kushirikishwa katika nyanja mbalimbali za uchukuaji maamuzi. Ukosefu wa wahudumu wa afya wanawake  na matabibu ulioshuhudiwa katika tetemeko la ardhi la hivi karibuni huko Afghanistan unaweka wazi umuhimu wa kupatiwa elimu wanawake ili kutoa huduma kwa wananchi wa Afghanistan; kwani  Taliban yenyewe imetambua vyema uhaba wa nguvu kazi hiyo ya kike. 

Wanawake wa Afghanistan na umuhimu wa kushirikishwa katika siasa na uchukuaji maamuzi chini ya utawala wa Taliban 

Farhad Abrar machambuzi wa Kiafghani anasema kuhusiana na hilo kwamba: "Loya Jirga hiyo ya Taliban haijakamilika, na maamuzi ndani ya baraza hilo yalishaamuliwa tangu huko nyuma". "Wanawake wa Afghanistan pia walitarajia kupewa heshima na baraza hilo."

Ala kulli hal, kufanyika kikao hicho cha siku tatu cha Loya Jirga ya maulamaa ingawa kunadhihirisha namna Taliban inavyojaribu kufikia mapatano ili kuunda serikali inayoitaka lakini kitendo cha kupuuza sehemu muhimu ya jamii ya Afghanistan katika mchakato huo kunakipa sura ya kimaonyesho tu kikao hicho; na bila shaka mtazamo kama huu hauwezi kufanikisha jitihada za kundi tawala la Taliban ili kutambuliwa kimataifa. Aidha ndani ya Afghanistan kwenyewe pia kundi tawala la Taliban linahitaji kustafidi na vipawa na nguvu kazi zote ndani ya nchi khususan kuwajumuisha wanawake katika nyanja za kisayansi, kielimu na katika kuchukua maamuzi; mambo ambayo hadi sasa yamepuuzwa na kundi hilo. 

Tags