Jul 03, 2022 07:56 UTC
  • HAMAS: Israel inapaswa kukabiliwa kwa jibu kali kwa kuishambulia Syria

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imelaani chokochoko mpya za Israel dhidi ya Syria na kusisitiza kuwa, utawala huo haramu unapaswa kukabiliwa kwa jibu kali kwa kuushambulia mji bandari wa Syria.

Msemaji wa HAMAS, Hazem Qassem alisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, Tel Aviv inadhihirisha hulka yake ya jinai kwa kushambulia maeneo ya Syria.

Qassem amenukuliwa na kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon akisema kuwa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Syria yamesadifiana na jitihada za baadhi ya madola ya eneo la Asia Magharibi, za kutaka kuunda muungano wa kijeshi yakishirikiana na Israel.

Ameeleza bayana kuwa, mpango huo wa kuunda eti NATO ya Mashariki ya Kati hauna dhamira nyingine isipokuwa kuhudumia maslahi ya utawala huo pandikizi, ya kuimarisha sera yake ya kujitanua katika eneo. 

Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina amesisitiza kuwa, kitendo cha Israel cha kushambulia kwa makombora mji bandari wa Tartus magharibi mwa Syria kinapaswa kupewa jibu mwafaka. 

Wanamapambano wa HAMAS

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, ametoa mwito kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuirejeshea Syria kiti chake cha uwanachama katika jumuiya hiyo.

Ramtane Lamamra alitoa mwito huo jana Jumamosi katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Arab League katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut na kueleza kuwa: Syria ni mwanachama mwasisi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, na Algeria haipingi kuirejeshea uanachama katika taasisi hiyo.

Tags