Jul 03, 2022 10:08 UTC
  • Tahadhari ya UN kuhusu maafa ya binadamu huko Ukanda wa Gaza

Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake kwamba kuzingirwa kwa miaka 15 kwa Ukanda wa Gaza kumesababisha maafa makubwa katika eneo hilo.

Tangu mwaka 2006 utawala wa Kizayuni wa Israel umeliweka eneo la Ukanda wa Gaza chini ya mzingiro wa pande zote. Sababu kuu ya mzingiro wa utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza ni ushindi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika uchaguzi wa Bunge la Palestina na kushindwa harakati ya Fat'h, na vilevile makubaliano ya kiusalama kati ya Misri na utawala wa Kizayuni. Ijapokuwa serikali iliyotokana na uchaguzi huo wa Bunge la Palestina ilisambaratika kutokana na mizozo ya ndani, na harakati ya Fat'h ikachukua tena madaraka, lakini mzingiro wa utawala wa Israel haujaisha na unaendelea hadi hii leo licha ya kupita miaka 15 sasa. 

Kutokana na mzingiro huo, Gaza imekumbwa na maafa makubwa. Kuzingirwa kwa miaka 15 eneo la Gaza kumesababisha uhaba wa chakula katika eneo hilo kiasi kwamba, Umoja wa Mataifa na Shirika la Chakula na Kilimo la umoja huo (FAO) pia wameeleza wasiwasi wao kuhusu suala hilo. Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Kisiasa na Kiuchumi cha Palestina, mwaka 2021 zaidi ya nusu ya familia za Wapalestina hazikuwa na usalama wa chakula.

Ukanda wa Gaza

Wakati huo huo Mpango wa Chakula Duniani (WFP) pia umetangaza mara kadhaa kuwa njaa na umasikini vinatishia maisha ya maelfu ya Wapalestina wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kutokana na siasa za utawala wa Kizayuni wa Israel. Takwimu zinaonesha kuwa, thuluthi mbili ya Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza walisumbuliwa na ukosefu wa chakula mwaka uliopita wa 2021 kutokana na mzingiro wa kidhalimu wa utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa eneo hilo. 

Mbali na uhaba wa chakula, Ukanda wa Gaza pia unasumbuliwa na hali mbaya ya huduma za tiba ya afya. Ni vyema kusema hapa kuwa, utawala wa Kizayuni wa Isarel pia umezuia kuigizwa dawa na vifaa vya matibabu katika eneo la Ukanda wa Gaza. Sambamba na kusumbuliwa na magonjwa hatari, maelfu ya watu Gaza wanazuiliwa kuondoka katika eneo hilo kwa ajili ya matibabu. Hata mgogoro wa maambukizi ya virusi vya corona pia haukuufanya utawala wa Kizayuni usitishe mzingiro wa pande zote dhidi ya Ukanda wa Gaza. Hapo awali msemaji wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu alitangaza kuwa, vikwazo vikali dhidi ya watu na bidhaa, mbali na mizozo ya ndani ya Palestina, vimeifanya hali ya wakazi wa Gaza kuwa mbaya na kuifanya eneo lililotengwa na ulimwengu; jambo ambalo limezidisha mbinyo na mashinikizo kwa uchumi wake. Kwa mfano tu huduma za kimsingi kama vile afya, maji na umeme huko Gaza zinakabiliwa na matatizo makubwa na wagonjwa wa Gaza hawawezi kuondoka katika eneo hilo kwa ajili ya matibabu bila ya kibali cha maafisa wa utawala wa Kizayuni.

Watoto wa Gaza wanaendelea kuuawa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa kuzingatia hali hiyo, Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu katika Maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu (OCHA) imetangaza katika ripoti yake kwamba hali ya Ukanda wa Gaza imekuwa ya maafa baada ya miaka 15 ya kuzingirwa eneo hilo kutokea nchi kavu, baharini na angani. Ripoti ya OCHA imesema: Kuzingirwa Ukanda wa Gaza kumeongeza hali ya umaskini na ukosefu wa ajira katika eneo hilo, kuharibu uchumi wa Wapalestina, na kuwafanya asilimia 50 miongoni mwao wategemee misaada ya kimataifa. Imesema mzingiro huo wa Israel umesababisha vifo vya maelfu ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.

Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, japokuwa Umoja wa Mataifa na taasisi zake zimeonya mara nyingi kuhusu maafa ya binadamu katika Ukanda wa Gaza, na hata Umoja wa Mataifa umelitaja eneo hilo kuwa "ni jela kubwa zaidi ya wazi duniani", lakini hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kushughulikia suala hilo na kwa ajili ya kukomesha mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.