Jul 03, 2022 11:15 UTC
  • Israel imewaua shahidi Wapalestina 77 katika kipindi cha miezi sita

Tokea mwanzo wa mwaka huu wa 2022, hadi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umewaua shahidi Wapalestina 77 wakiwemo watoto 15.

Mohammad Sabihat Katibu Mkuu wa Taasisi ya 'Mjumuiko wa Kitaifa wa Familia za Mashahidi wa Palestina', ametoa taarifa leo na kusema kuwa utawala katili wa Israel mwaka huu tayari umeshawaua shahidi Wapalestina 77 wakiwemo watoto 15. 

Taarifa hiyo imebaini kuwa kuongezeka idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi, hasa watoto ni ishara ya kushadidi jinai za kigaidi za utawala wa Kizayuni.

Mtoto Mpalestina mwenye umri wa chini zaidi aliyeuawa shahidi ni Mohammad Rizq Shahad Zalah aliyekuwa na umri wa miaka 14 na ambaye aliuawa shahidi Februari 23 katika eneo la Beit Lahm na mwenye umri wa juu zaidi kuuawa shahidi ni Umar Abdul Majid Asa'ad aliyekuwa na umri wa miaka 80 ambaye aliuawa shahidi Januari 12 mjini Ramallah.

Nacho Kituo cha Habari cha Muata cha Palestina kimechapisha ripoti inayoonyesha kuwa, maeneo ya Ukingo wa Magharibi na mji wa Quds (Jerusalem) katika mwezi uliopita wa Juni yalishuhudia matukio 649 ya Wapalestina kutekeleza oparesheni za kimapambano ambapo Wazayuni 26 walijeruhiwa.

Askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakimkamata mtoto Mpalestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitekeleza jinai kwa lengo la kujitanua zaidi katika ardhi za Wapalestina na hivyo kupelekea idadi kubwa ya Wapalestina kuuawa shahidi na kujeruhiwa wakiwemo watoto wasio na hatia. 

Juzi Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa alisema, ukatili mtawalia na wa kimfumo ambao utawala haramu wa Kizayuni wa Israel unawafanyia Wapalestina ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Katika ujumbe aliomtumia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na marais wa Baraza la Usalama na Baraza Kuu la umoja huo, Riyadh al Mansour ameeleza kwamba, ukatili mtawalia na wa kimfumo ambao utawala haramu wa Kizayuni unawafanyia Wapalestina ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa likiwemo azimio 2234 la Baraza la Usalama ambalo limetaka zichukuliwe hatua za haraka za kuzuia aina zote za utumiaji mabavu na kufanya ukatili dhidi ya raia.

Tags