Jul 04, 2022 14:08 UTC
  • Balozi wa Syria Moscow: Magharibi na Uturuki zinawatuma wapiganaji wa ISIS nchini Ukraine

Balozi wa Syria nchini Russia amesema kuwa Damascus ina habari kwamba nchi za Magharibi na Uturuki zinatuma wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Ukraine.

Riyad Haddad, balozi wa Syria nchini Russia amesema katika mazungumzo yake na shirika la habari la Tass kwamba: "Hatushangai kwamba Marekani, nchi za Magharibi na Uturuki zinatuma wanamgambo wa makundi ya kigaidi ya ISIS na Jabhat al-Nusra kutoka Idlib kwenda Ukraine, na makundi haya, ingawa yanapewa majina tofauti, lakini yanatumiwa kama chombo cha Magharibi dhidi ya mataifa yanayopigania amani.

Mwanadiplomasia huyo wa Syria ameongeza kuwa, "Hivi ndivyo wanavyoigeuza Ukraine kuwa kituo cha magaidi na makundi ya mamluki, bila kujali matokeo mabaya ya sera hiyo kwa usalama wa kimataifa."

Siku chache zilizopita pia shirika la habari la Sputnik limeripoti kuwa, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) linawasajili magaidi wa Daesh (ISIS) ili wapelekwe Ukraine kwa kisingizio cha vita nchini humo.

Sputnik imeripoti kuwa, shirika la ujasusi la CIA linasajili magaidi wa ISIS katika magereza au maficho yao eneo la Asia Magharibi ili kuwapeleka kupigana Ukraine kama mamluki.

Ripoti hiyo inakuja wakati Idara ya Usalama wa Nje ya Nchi ya Russia- SVR RF- imefichua kuwa, Marekani inawasafirisha magaidi wa ISIS au Daesh kutoka Syria na kuwaingiza Ukraine.

ISIS

Taarifa ya SVR-RF imesema magaidi hao wa ISIS wamekuwa wakipata mafunzo maalumu katika kituo kimoja cha kijeshi kilicho Syria kinyume cha sheria na baada ya kupata mafunzo wanaepelekwa Ukraine.

Taarifa hiyo imesema: "Mwishoni mwa mwaka 2021, Marekani iliwaachilia huru wafungwa wakiwemo makumi ya magaidi wa ISIS, na miongoni mwao walikiwemo raia wa Russia na nchi za CIS. Watu hawa walipelekwa katika kituo cha kijeshi cha al Tanf kinachosimamiwa na Marekani ambapo wamepewa mafunzo maalumu ya mbinu za kigaidi za vita na wametumwa eneo la Donbass."