Jul 05, 2022 00:56 UTC
  • Matamshi ya Fuad Hussein kuhusu upatanishi wa Iraq kati ya Iran, Misri na Jordan

Matamshi ya hivi karibuni ya Fuad Hussein, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq katika mahojiano na televisheni ya Saudi Arabia ya al-Arabiya kuhusu upatanishi wa nchi hiyo kati ya Iran, Misri na Jordan ni ya kuzingatiwa.

Fuad Hussein ametoa matamshi hayo katika hali ambayo hakuna nchi yoyote kati ya nchi hizo tatu ambayo imezungumzia suala hilo, na kabla ya hapo pia, hakuna habari yoyote iliyotangazwa inayoonyesha kuwa Iraq imekuwa ikifanya juhudi za aina hiyo katika uwanja huo. Kimsingi uhusiano wa Iran na Misri na Jordan kwa miaka na miongo ya hivi karibuni haujafikia kiwango ambacho kinahitajia kufanyika upatanishi wa kuondoa mvutano, na ingawa nchi hizi hazijakuwa na uhusiano mzuri sana kikanda, lakini hazijawahi kuwa na makabiliano ya moja kwa moja. Licha ya kuwa na tofauti za kisiasa lakini nchi tatu hizi zimeweza kutekeleza siasa zao za nje kwa namna ambayo inaepusha mivutano na makabiliano.

Kwa kuzingatia historia hiyo, inashangaza kuona kwamba kauli hiyo imetolewa ghafla na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq tena katika mahojiano na televisheni ya al-Arabiya ya nchini Saudia. Kwa hakika, kile kinachostahili kuzingatiwa zaidi ni kuakisiwa pakubwa kauli hiyo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq na televisheni ya al-Arabiya na kisha katika vyombo vingine vya habari vya kieneo na kimataifa vya nchi za Magharibi kama vile BBC.

Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq

Kwa kuzingatia hilo, kutolewa matamshi hayo kunakwenda sambamba na maslahi ya kisiasa ya Saudi Arabia kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, kunathibitisha kuendelezwa siasa ambazo amekuwa akizitekeleza Mustafa al-Kadhimi Waziri Mkuu wa Iraq tangu aingie madarakani kwa ajili ya kuifanya nchi hiyo kuwa mpatanishi muhimu katika migogoro ya kieneo.

Kuhusu mahitaji ya kisiasa ya Saudi Arabia, tunaweza kusema kuwa nchi hiyo ya kifalme inakabiliwa na mashinikizo makubwa kutoka kwa utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuanzisha na kuweka wazi uhusiano wake na utawala huo ghasibu wa Kizayuni, lengo ambalo limepangwa kufikiwa katika safari ijayo ya Rais Joe Biden wa Marekani huko Israel na Saudi Arabia. Pamoja na hayo lakini Saudia ina wasiwasi wa kuharibika jina lake katika ulimwengu wa Uislamu kutokana na uhusiano huo na ndio maana inatumia mpango wa upatanishi wa Iraq kati ya Misri na Jordan, ambazo tayari zimetia saini mikataba ya amani na utawala ghasibu wa Israel, kama mbinu ya kipropaganda katika uwanja huo.

Wakati huo huo, mwishoni mwa utawala wa Donald Trump huko Marekani ambao pia ni wakati wa kuingia madarakani serikali ya Mustafa al-Kadhimi huko Iraq, juhudi nyingi zimekuwa zikifanywa kwa ajili ya kuisukuma nchi hiyo mikononi mwa utawala wa Kizayuni, lakini juhudi hizo zimefeli kutokana na upinzani mkali uliojitokeza ndani ya nchi hiyo hususan kutoka kwa vyama na makundi ya Kishia. Kwa hivyo katika hatua ya kwanza, kundi linalojulika kama Bilad Sham, ambalo linajumuisha Iraqi na nchi mbili za Misri na Jordan, limeundwa kati ya nchi hizo na tayari mikutano kadhaa imefanyika ili kuratibu na kufuatilia malengo yanayokusudiwa kufikiwa katika uwanja huo. Imeamuliwa kuwa Iraq itazipatia nchi mbili hizo mafuta ya bure au kwa bei nafuu.

Bunge la Iraq lililopiga marufuku kuanzishwa uhusiano na utawala haramu wa Israel

Hata hivyo, kwa kuzingatia sheria ambayo ilipitishwa hivi karibuni na bunge la Iraq, ya kupiga marufuku na kuchukulia kuwa hatia kuanzishwa uhusiano wa aina yoyote na utawala haramu wa Israel, itakuwa vigumu kwa nchi mbili hizo za Kiarabu kuanzisha uhusiano huo na utawala wa kibaguzi wa Israel kwa kutumia visingizio tofauti kama vile vya Iraq kuwa mpatanishi kati ya Iran, Misri na Jordan, kama tulivyoshuhudia  hilo kupitia kauli iliyotolewa na Fuad Hussein katika mazungumzo yake na televisheni ya al-Arabiya.