Jul 05, 2022 07:35 UTC
  • Silaha ya Muqawama, dhamana pekee ya kupata maslahi ya Lebanon katika medani ya gesi ya Karish

Jumamosi iliyopita harakati ya Hizbullah ya Lebanon ilirusha ndege tatu zisizo na rubani katika anga eneo lenye utajiri wa gesi la Karish.

Eneo hili lina futi za ujazo trilioni 203 za gesi, na utawala wa Kizayuni wa Israel unataka kulidhibiti na kuwa muuzaji wa gesi badala ya mtumiaji tu wa nishati hiyo na kulitumia kama nyenzo ya kisiasa na kiuchumi katika fremu ya sera zake za kupenda kujitanua.

Utawala huo ghasibu unatumia haja kubwa ya nchi za Magharibi, hasa Ulaya, kwa nishati ya gesi hususan baada ya kutokea vita vya Ukraine ambavyo vimepelekea kupungua kwa mauzo ya gesi ya Russia, kama fursa ya kufikia malengo yake, na kwa njia hii, unataka kuzivutia upande wake nchi hizo za Maghahribi katika kakdhia hiyo. Katika mkondo huo, hivi karibuni Israel ilifunga mkataba na kampuni ya Kiingereza-Kigiriki wa kuchimba gesi katika eneo la baharini la Karish, lakini imechukua dhamana ya kulinda usalama wa eneo hilo. Hata hivyo, baadhi ya vyanzo vya habari vinaonesha kuwa jukumu hilo limekabidhiwa kwa Marekani na kwamba meli mbili za kivita za Marekani zimewekwa katika eneo hili linalozozaniwa. Iwapo habari hii itakuwa ya kweli, itazidisha umuhimu wa kitendo cha harakati ya Hizbullah ya kutuma ndege tatu zisizo na rubani za upelelezi kwenye eneo hilo, na kinaonesha kwamba Hizbullah haitaacha kutekeleza wajibu wake katika uwanja huu kwa hali yoyote ile.

Medani ya gesi ya Karish

Kabla ya uvamizi na uchokozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika medani ya gesi ya Karish na maeneo mengine yenye mgogoro yenye ukubwa wa karibu kilomita za mraba 1400, wapinzani wa ndani na nje wa Hizbullah daima walikuwa wakisisitiza kwamba, hakuna haja ya kuwepo silaha za Hizbullah na kwamba harakati hiyo lazima ipokonywe silaha. Hata hivyo visingizio hivyo vya wapinzani wa Hizbullah sasa vimesambaratika na kukosa mashiko, na umuhimu wa kuendelea kulindwa silaha na zana za kivita za harakati hiyo ya muqawama umeonekana vyema zaidi kwa wananchi, serikali ya Lebanon na hata mbele ya wapinzani na washindani wa Hizbullah.  

Licha ya tofautia za kimaoni zinazoshuhudiwa ndani ya Lebanon, lakini tunaweza kusema kwamba, Walebanoni wengi wanakubaliana kwamba, kama zilivyo nchi nyingine, wanaweza kufaidika na rasilimali na akiba yao ya nishati ili kuondokana na umaskini uliokithiri na migogoro ya kiuchumi. Si hayo tu bali hata wale waliokuwa wametegemea na kuamini upatanishi wa Marekani katika kadhia hiyo wameshuhudia kwa macho wao wenyewe jinsi Washington- kama kawaida yake- ilivyoupendelea utawala wa Kizayuni wa Israel, na hata baadhi ya ripoti zinasema, imeamua kutuma manuwari mbili za kivita kusimamia kazi ya Israel ya kuchimba gesi katika eneo hilo linalogombaniwa. 

Wakati huo huo, serikali ya Lebanon imelipa kipaumbele maalumu suala la kufaidika na rasilimali zake za gesi na mafuta, na Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati, pia ametangaza kuwa suala hilo ni moja ya vipaumbele vya serikali yake.

Najib Mikati

Hata hivyo inatupasa kuelewa kuwa Lebanon haina dhamana yoyote ya kulinda na kutetea rasilimali zake hizo isipokuwa silaha za harakati ya Hizbullah. Ni Kwa mtazamo huo, ndio maana tukasema kuwa, uvamizi wa Israel katika medani ya gesi ya Lebanon unazidisha mara dufu umuhimu na ulazima wa kudumishwa silaha za Hizbullah na umebatilisha propaganda zote chafu na porojo za kisiasa zilizofanywa kwa miongo kadhaa ya hivi karibuni dhidi ya harakati hiyo ya Kiislamu. Hii ni pamoja na kuwa, uvamizi huo unaanda misingi ya kisheria ya haki ya kujitetea ya Lebanon na Hizbullah.