Jul 06, 2022 08:49 UTC
  • Waziri wa Utamaduni wa Yemen: Mamluki wa Saudia wanaiba athari za kale za Yemen

Waziri wa Utamaduni wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ametangaza kwamba mamluki wa Saudi Arabia na washirika wake wanajaribu kupora athari za kale za nchi hiyo.

Abdullah Ahmad al-Kibsi, Waziri wa Utamaduni wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen, amesema mamluki wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudia wanafanya juhudi za kuiba vitu na athari za kale na kuharibu maeneo ya kihistoria katika mikoa yote ya Yemen, na ameliomba Shirika ya Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuzuia uuzwaji wa athari za kale za Yemeni katika masoko ya Ulaya na Marekani.

Ahmad al-Kibsi asema kuwa muungano wavamizi na mamluki wake hawakutosheka na kushambulia maeneo ya kale na ya kihistoria na kupora athari za kale katika mikoa inayokaliwa kwa mabavu, bali unatumia vifaa vya kugundua chuma ili kupora na kuiba athari za kale na kuharibu maeneo ya kihistoria katika mikoa iliyokombolewa ya Yemen.

Hapo awali, mtandao wa Saudi WikiLeaks ulikuwa umeandika katika ripoti yake kwamba waraka uliofichuliwa hivi karibuni kutoka taasisi ya kupambana na ufisadi ya Saudi Arabia unaonyesha kuwa mtandao unaofungamana na Muammar Al-Ariani, aliyekuwa waziri wa habari wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen, unafanya magendo ya athari za kale za Yemen na kuziuza kwenye soko la Ulaya kupitia Saudi Arabia.