Jul 06, 2022 08:50 UTC
  • Jihad Islami: Ripoti ya Marekani kuhusu mauaji ya Abu Akleh inaficha uhalifu wa Israel

Harakati ya Jihad ya Islami ya Palestina imetangaza kuwa, ripoti ya Marekani kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari wa al Jazeera, Shireen Abu Akleh ni ya kisiasa na imechapishwa kwa shabaha ya kuuondoa hatiani na kuficha jinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Jumatatu iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilidai katika ripoti iliyolenga kuiondolea mashtaka Tel Aviv kwamba "Shireen Abu Akleh huenda aliuawa bila kukusudia kwa risasi iliyotoka upande wa wanajeshi wa Israel."

Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imesisitiza katika taarifa yake kwamba, ripoti ya upendeleo ya Marekani kuhusu utawala wa Kizayuni wa Israel imetolewa ndani ya fremu ya mienendo ya kawaida ya Marekani ya kumuunga mkono adui Mzayuni, na hata inaweza kusemwa kuwa, Washington inahusika katika mauaji na ugaidi unaofanywa dhidi ya wananchi wa Palestina kupitia misaada yake ya silaha za aina mbalimbali kwa utawala huo ghasibu.

Taarifa ya Jihad Islami pia imelaani hatua ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kukubali kushirikishwa Marekani katika uchunguzi kuhusiana na mauaji ya mwandishi wa habari wa televisheni ya al-Jazeera na kuikabidhi Washington risasi zilizomuua mwanahabari huyo.

Hapo awali, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) nayo pia ilitoa taarifa ikilaani matokeo ya uchunguzi wa Marekani kuhusu mauaji ya mwandishi habari wa al Jazeera, Shireen Abu Akleh yaliyofanywa na jeshi la Israel. Hamas ilitangaza kuwa matokeo yaliyotangazwa na Marekani yanaunga mkono waziwazi maelezo yaliyotolewa na utawala wa Kizayuni juu ya mauaji hayo na ni jaribio la kuwaondoa hatiani Wazayuni na kuwavua lawama za kuhusika na jinai hiyo ya kutisha.

 Shireen Abu Akleh

Wakati huo huo viongozi wa Palestina wameituhumu serikali ya Marekani kuwa imefanya kila iwezalo kuukingia kifua utawala ghasibu wa Israel katika jinai hiyo.

Shireen Abu Akleh aliyekuwa na umri wa miaka 51, ripota wa televisheni ya al Jazeera yenye makao yake nchini Qatar, aliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel tarehe 11 mwezi Mei mwaka huu wakati akiripoti  uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa al Aqsa.